
Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA AFRICA KUSINI
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma amesema kuwa Serikali iko bega kwa bega na vilabu vya mpira wa miguu kuhakikisha michezo nchini inapata hadhi inayostahili.
Mhe. Mwinjuma amesema hayo wakati akiwapongeza Simba SC baada ya kufuzu kutinga fainali ya kombe la Shirikisho la Afrika ( CAFCC), Aprili 27, 2025 nchini Afrika kusini walipokuwa wakichuana na mwenyeji wake Stellenbosch.
“Tunafahamu kuwa huu mchezo una wapenzi wengi, hivyo sisi kama Serikali tunafanya kile kilicho ndani ya uwezo wetu kuhakikisha hatuwaangashi wapenzi wa soka nchini” amesema Mhe. Mwinjuma.
Aidha, Mhe. Mwinjuma amebainisha kuwa soka la Tanzania limepanda kwa kiasi kikubwa na timu hizo sasa zinafika mashindano makubwa na kupambana hadi kufikia hatua za juu zaidi.
“Mpira wetu umepanda kweli, kuna uwezekano mkubwa safari hii tukawa mabingwa wa kombe hili, tuache figisufigisu, tuombeane Mungu, hii ni kwa ajili ya Tanzania n ani Oparesheni ya nchi” amesema Mhe. Hamis Mwinjuma.
Katika hatua nyingine, Mhe. Mwinjuma amewataka Watanzania kutambua kuwa soka la mpira wa miguu nchini limepanda na kufikia hatua kubwa hivyo kusherehekea mafanikio ambayo timu zetu zinafikia.