21 views 2 mins 0 comments

TANESCO YAANZA RASMI ZOEZI LA KULIPA FIDIA WANANCHI WALIOPISHA UJENZI WA MIRADI YA UMEME

In KITAIFA
April 27, 2025



Mtwara, Ruvuma

📌Ni mradi wa ujenzi wa njia kubwa ya kusafirisha umeme wa kilovoti 220 Tunduru -Masasi .

📌Jumla ya shilingi Bilioni 4.7 kutumika kulipa fidia  kwa wananchi

📌Wananchi waahidi kuyahama maeneo  ndani ya siku 30 walizopewa.

Jumla ya wananchi 1,526  wanatarajia kunufaika na malipo ya fidia ya shilingi Bilioni 4.7 baada ya kupisha Mradi wa ujenzi wa njia kubwa ya kusafirisha umeme wenye msongo wa Kilovoti 220 kutoka Tunduru hadi Masasi na ujenzi wa Kituo kipya cha kupoza umeme cha Masasi kilichopo Mkoani Mtwara.

Akizungumza baada ya wananchi kukabidhiwa hundi  April 26, 2025  Mwenyekiti wa Kijiji cha Sululu Venant Kamtahule  licha ya kulishukuru Shirika la Umeme Tanzania TANESCO kwa ajili ya malipo hayo, wamesema ujenzi wa miradi hiyo imelenga kuimarisha upatikanaji wa umeme utakaochochea shughuli za kiuchumi na uwekezaji wa viwanda vya kubangua korosho.

‘’Kiukweli tunaishukuru sana TANESCO wananchi wangu takribani 16 wa Kijiji cha Sululu wamenufaika na malipo ya fidia, haya ni mafanikio  makubwa tuliyokua tukiyasubiria kwa muda mrefu .Tunaimani mradi huu utaongeza chachu ya upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa  wananchi,’’ alifafanua ndugu Venant

Naye Meneja wa TANESCO Wilayani Masasi Mhandisi Kidala Maeda amesema zoezi hilo la ulipwaji fidia limeanza tangu April 25, 2025 ambapo amefafanua kuwa hatua hii itamuwezesha Mkandarasi kuendelea na ujenzi hususani katika Kituo cha kupoza umeme cha Masasi ambao utekelezaji wake uko katika hatua za awali.


‘’Kama mnavyojua hii Mikoa miwili ya Lindi na Mtwara bado haijaunganishwa na Gridi ya Taifa tunatumia mashine za gesi kutoka Mtwara, lakini Serikali ikaona  ni wakati sasa na sisi watu wa Kusini tupate umeme kupitia Gridi ya Taifa ili tunufaike na umeme unaozalishwa kutoka Mradi wa kufua umeme wa bwawa la Julius Nyerere ambao umekamilika rasmi’’ alisisitiza Mha. Kidala.

Mradi wa njia kubwa ya kusafirisha umeme wenye msongo wa  Kilovoti 220 kutoka Tunduru hadi Masasi na ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Masasi utagharimu zaidi ya shilingi bilioni 70 ambapo jumla ya vijiji 43 vinapitiwa na Mradi huo katika Wilaya za Masasi, Nanyumbu na Tunduru.

/ Published posts: 1972

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram