

NA MWANDISHI WETU
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), kwa kushirikiana na vyombo mbalimbali vya dola, imefanikiwa kukamata jumla ya kilogramu 4,568 za dawa za kulevya, kuteketeza ekari 178 za mashamba ya bangi na magari saba, pikipiki tano na bajaji moja zimekamatwa kwa kuhusika katika shughuli za usafirishaji wa dawa hizo.
Hayo yamebainishwa leo Aprili 24, 2025 na Kamishna Jenerali wa DCEA Aretas Lyimo akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam ambapo ameeleza kuwa walifanya ukamataji huo baada ya kufanya oparesheni kubwa katika mikoa kadhaa ya Tanzania na kufanikisha kukamatwa kwa kiasi hicho kikubwa cha dawa za kulevya, kemikali bashirifu, magari na watuhumiwa waliokuwa wanajihusisha na biashara hiyo haramu.
Kamishna Lyimo amebainisha kuwa operesheni hizo zilifanyika kati ya Machi na Aprili mwaka huu katika mikoa ya Dar es Salaam, Shinyanga, Tabora, Tanga, Songwe, Mbeya na Arusha.
Kwamba watuhumiwa 35 wamekamatwa kutokana na matukio hayo na hatua za kisheria zinaendelea dhidi yao.
Katika hatua nyingine, amesema DCEA kwa kushirikiana na Bodi ya Kimataifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya (INCB) imefanikiwa kuzuia tani 14 za kemikali bashirifu kuingia nchini kinyume cha sheria.
Amesema Kemikali hizo ni pamoja na kilogramu 4,000 za 1-Boc-4-piperidone na kilogramu 10,000 za acetic anhydride, zilizotakiwa kuingizwa kutoka Bara la Asia bila kuwa na vielelezo halali vya matumizi.
Kwamba kiasi hicho cha kemikali kingeweza kutumika kuzalisha kilogramu 8,000 za dawa aina ya fentanyl, ambayo kiasi kidogo tu cha miligramu mbili kinaweza kusababisha kifo kwa mtu mmoja.
Hivyo, fentanyl iliyoweza kuzalishwa ingeweza kusababisha vifo vya watu bilioni 4. Acetic anhydride nayo ingeweza kutumika kutengeneza kilo 3,704 za heroin au kemikali nyingine hatari kama methamphetamine na mandrax.
Amesema katika tukio jingine mkoani Mbeya, raia wa Uganda Herbert Kawalya alikamatwa akiwa na pakti 10 za pipi zenye uzito wa gramu 174.77 zilizotengenezwa kwa bangi yenye kiwango kikubwa cha sumu aina ya THC.
Aidha, gari aina ya Mercedes Benz iliyokuwa ikisafirisha pipi hizo kutoka Afrika Kusini nayo ilikamatwa. Pia, mkoani humo zilikamatwa kilo 1,658 za bangi aina ya skanka na kilo 128.7 zilizokuwa zikiingizwa kutoka Malawi.
Kwa upande wa jijini Dar es Salaam, operesheni iliyoendeshwa katika kata ya Chanika ilikamata kilo 220.67 za bangi aina ya skanka zilizofichwa chooni, na kilo 11 nyingine zilipatikana katika eneo la ukaguzi wa mizigo bandarini kuelekea Zanzibar.
Kwamba katika mikoa ya Arusha, Tanga, na Manyara zilikamatwa kilo 733.74 za methamphetamine, kilo 91.62 za heroin, kilo 692.84 za mirungi kutoka Kenya na kilo 115.05 za bangi, pamoja na kuteketeza ekari mbili za mashamba ya bangi. Mkoani Tabora wilaya ya Uyui na Nzega, kilo 845 za bangi zilipatikana na ekari 176 za mashamba ya bangi zilibomolewa. Shinyanga na Kahama walinaswa na kilo 98.35 za bangi.
Ameeleza kuwa mafanikio haya yametokana na ushirikiano wa karibu na taasisi za ndani na nje ya nchi, na yamezuia athari kubwa kiafya, kijamii, kiuchumi na kimazingira ambazo zingeletwa na dawa hizo mitaani. Hii ni pamoja na kuokoa maisha ya mamilioni ya vijana ambao wangepotea kutokana na matumizi ya dawa hizo.
Ametoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana kwa kutoa taarifa mapema kuhusu shughuli za uzalishaji au biashara ya dawa za kulevya kwa kupiga simu bure namba 119. Wazazi na walezi pia wamehimizwa kuwa makini na mienendo ya watoto wao na kuwapa elimu kuhusu madhara ya dawa za kulevya.
Kwa upande mwingine, kampuni zinazotumia kemikali za viwandani na kilimo zimekumbushwa kuzingatia sheria na kuepuka kushirikiana na magenge ya kihalifu yanayochepusha kemikali hizo kwa ajili ya kutengeneza dawa za kulevya.