
Dar es Salaam.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imepokea timu ya wataalamu kutoka Ofisi za Umoja wa Afrika (AUC) wanaoratibu utekelezaji wa mradi wa kuboresha huduma za hali ya hewa wa “Intra-ACP Climate Services and related Applications Programme (ClimSA)”.
Ziara hiyo ilifanyika tarehe 17 Aprili, 2025 ikioongozwa na mmoja wa Wasimamizi wa mradi wa ClimSA kutoka AUC Bw. Freddy Falanga (ambaye ni rai wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo), ambapo timu hiyo ya wataalamu walitembelea Ofisi Kuu ya Utabiri wa Hali ya Hewa, iliyopo Ubungo Plaza, Dar es salaam kwa lengo la kukagua utendaji kazi wa mitambo ya ufuatiliaji wa mifumo ya hali ya hewa na utabiri wa hali ya hewa, inayoitwa “PUMA STATION.”, iliyotolewa kwa TMA kupitia mradi ClimSA.
Mradi wa ClimSA unatekelezwa katika nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AUC), ikiwemo Tanzania kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya (European Union). Mradi huu unalenga kuimarisha zaidi uwezo wa nchi wanachama wa AU katika kufuatilia mifumo ya hali ya hewa kupitia teknolojia ya satelaiti ili kuboresha zaidi utabiri wa hali ya hewa na huduma za hali ya hewa kwa ujumla.
Huduma hizi ni muhimu kwa jamii na sekta za kiuchumi katika kupanga shughuli za maendeleo na kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi.