7 views 3 mins 0 comments

ULEGA ATOA SIKU 30 KWA MKANDARASI BARABARA YA NSALAGA – IFISI KUWEKWA LAMI

In KITAIFA
April 22, 2025

Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA

Waziri wa Ujenzi,  Abdallah Ulega ametoa siku 30 na kumtaka Mkandarasi Kampuni ya CHICO anayetekeleza ujenzi wa upanuzi wa barabara ya Nsalaga – Ifisi (km 29) kwa njia nne, jijini Mbeya kuongeza kasi ya ujenzi wa mradi huo ili uweze kukamilika na kupunguza msongamano wa magari katika jiji hilo.

Aidha, Waziri Ulega amemuagiza Mkandarasi huyo kufanya kazi usiku na mchana, kuongeza vifaa pamoja wafanyakazi ili kufanikisha mradi huo ukamilike haraka iwezekanavyo.

Ulega ametoa maelekezo hayo jijini Mbeya wakati alipokuwa akikagua maendeleo ya mradi huo na kutoridhishwa na hatua za utekelezaji wake ambao hadi sasa umefikia asilimia 25.

Ulega ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tayari imeshatoa malipo ya Shilingi Bilioni 35 kwa Mkandarasi huyo na matarajio yake ni kuona kupitia fedha hizo angalau kilometa kadhaa za lami zimekamilishwa kujengwa katika barabara hiyo.

“Serikali imeshatoa Bilioni 35 kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii kutoka Nsalaga hadi Ifisi, na fedha hizi Mkandarasi hajazifanyia kazi ipasavyo, Sasa basi Nimemuagiza Mkandarasi afanye kazi usiku na mchana na kuona mabadiliko ya haraka katika mradi huu”, amesisitiza Ulega.

Pia,  ametoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Mbeya kumsimamia Mkandarasi kwa ukaribu ili hadi kufikia mwanzoni mwa Mwezi Juni mwaka huu Mkandarasi awe amekamilisha  kilometa 10 za lami katika barabara hiyo na kuahidi kurudi tena kwa ajili ya kukagua maendeleo hayo.

Ulega amemuelekeza Meneja huyo wa TANROADS kuhakikisha ujenzi wa barabara hiyo unaenda sambamba na ufungaji wa taa za barabarani ili kuupendezesha mji wa Mbeya na kuimarisha masuala ya ulinzi na usalama wa wananchi wanaotumia barabara hiyo katika shughuli zao za kiuchumi za kila siku.

Vilevile, Ulega amepokea Ombi la Mbunge wa Mbeya Mjini na Spika wa Bunge la Tanzania, Dkt. Tulia Ackson la ujenzi wa kilometa tano za lami zinazoingia katika mitaa ya iiji la Mbeya na kuahidi kulifanyia kazi.

Kadhalika, Ulega amemuagiza Meneja wa TANROADS mkoa wa Mbeya kumsimamia Mkandarasi katika kuhakikisha kazi ndogondogo   zinazofanywa na Mkandarasi zinatolewa kwa vijana wa Mkoa wa Mbeya ili kutoa fursa za ajira  na vijana hao waweze kunufaika na matunda ya mradi.

kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini na Spika wa Bunge  la Tanzania, Dkt. Tulia Ackson ameeleza kuwa wananchi wa Mbeya wamekuwa wakisubiri kwa hamu upanuzi wa barabara hiyo kukamilika ili kutatua changamoto za msongamano wa magari jijini humo.

Dkt. Tulia ameiomba Wizara ya Ujenzi kufanyia kazi mapendekezo yaliyoombwa katika barabara hiyo ya kuongezwa kwa barabara kilometa 3.5 kuanzia Ifisi hadi Songwe Airport na kilometa 5 kuanzia Nsalaga kuelekea Mlima Nyoka katika Bajeti mpya ya mwaka 2025/26 ili wananchi wa Mbeya kuendelea kunufaika na ujenzi wa mtandao wa barabara jijini humo.

Naye, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mbeya, Eng. Matari Masige ameeleza kuwa Mkandarasi anaendelea na ujenzi wa matabaka ya udongo G3, G7 na  G15, ujenzi wa makalvati madogo na makubwa pamoja na ujenzi wa daraja la Nzovwe katika barabara hiyo.

/ Published posts: 1941

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram