26 views 3 mins 0 comments

GAVANA BWANKU AONGOZANA NA WATENDAJI KUKAGUA UJENZI WA DARAJA KUBWA LA KISASA LA KALEBE

In KITAIFA
April 19, 2025

Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA

_Ni Daraja linalotesa Wananchi wakati wa mvua, Rais Samia aidhinisha Bilioni 9.7 linajengwa jipya la kisasa. Kukamilika Novemba._

Hakuna cha Jumamosi wala Jumapili, Katerero ni kazi juu ya kazi. Mchana wa leo Jumamosi Aprili 19, 2025 Afisa Tarafa ya Katerero iliyopo Bukoba mkoani Kagera Ndugu Bwanku M Bwanku akiongozana na Kaimu Mtendaji wa Kata ya Katerero Bi. Julie Kushoka na Mtendaji wa Kijiji Kyema Ndugu Najim Abbas wametembelea kukagua na kujionea ujenzi unaoendelea wa Daraja kubwa na la kisasa la Kalebe linalokatisha Mto Ngono litakalokuwa na Mita 60 na barabara ya kuunganisha Daraja Mita 750 pande zote mbili.

Eneo hili limetesa wananchi sana kwa miaka mingi hasa nyakati za mvua kubwa ambapo Daraja la sasa linalotumika hujaa maji na wananchi kushindwa kupita vyema hali inayowalazimu wananchi wa kata zaidi ya 20 za Bukoba Vijijini kuzunguka barabara ndefu ya Kamachumu na Kyaka ili kuingia Bukoba mjini na kutoka mana maji hufunika Daraja lote.

Hivyo Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imeamua kujenga Daraja jipya hili litakalokuwa la kisasa, refu na pana zaidi kwa magari kupishana na watu na ambalo hata mvua inyeshe kubwa kiasi gani wananchi watapita bila shida yoyote ile.

Daraja hili la kisasa linajengwa hapohapo lilipo Daraja la sasa la Kalebe likiwa katikati ya kata ya Katerero pamoja na kata ya Ibwera na Nyakibimbili. Litakamilika mwezi Novemba mwaka huu 2025 baada ya kuanza kujengwa Novemba mwaka jana 2024 na Mkandarasi Kampuni ya Milembe Construction kwa muda wa miezi 12 ya mkataba.

Afisa Tarafa Bwanku na ujumbe wake walipokelewa na Injinia Titus wa vifaa vya ujenzi , Mwakilishi wa TANROAD kwenye mradi Eng Alex Konakuze na Mpimaji (Surveyor) Eng Richard Palangyo, Afisa Usalama mahali pa kazi Desy Mallya na kukuta wasimamizi wa mradi, mafundi na mitambo mikubwa mbalimbali kama gari za kushindilia, gari za kusomba maji, Excavator, roli za kusomba vifusi na mchanga zaidi ya 5 zikiwa kazini kuendelea na ujenzi.

Ujenzi wa Daraja hili la Kalebe unaenda sambamba na ujenzi wa Daraja la Kyanyabasa ambalo lipo upande wa pili wa Mto Ngono kuunganisha kata ya Bujugo na Kishogo ambalo nalo ujenzi unaendelea kwa Bilioni 9.3. Eneo hili limetesa sana wananchi hadi sasa alipoingia Rais Samia kujenga madaraja yote mawili kwa mpigo ili kuondoa changamoto hii, madaraja yote yatakamilika Novemba mwaka huu 2025.

/ Published posts: 1934

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram