
Na Mwandishi Wetu
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Stephen Wasira amewahakikishia Watanzania kwamba Chama hakina chuki wala kısası na mtu bali kinaamini kutekeleza sera ya maridhiano.
Wasira ametoa kauli hiyo jana akiwa katika mkutano wa hadhara alipokuwa akizungumza na wana CCM wilayani Urambo mkoani Tabora ambako anaendelea na ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi, kuzungumza na viongozi wa CCM na kusikiliza kero za wananchi.
Alisema CCM inaamini katika maridhiano ambayo pia ni sera ya serikali chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ndio maana hata Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu alipokuwa amekimbia nchi, maridhiano ndiyo yalimrudisha nchini.
“Yule bwana mwenye kuuliza na wengine mliokuwa mnamsikiliza niwasaidie tu kuwaelimisha kwamba mkiwa na sera ya maridhiano haiwi mbadala wa sheria na wala huwezi kusema kwa sababu wewe ni mwenyekiti basi upo juu ya sheria.
“Wote tuko chini ya sheria hata mimi nikiamka sasa hivi nikakupiga kofi, Jeshi la Polisi watanikamata hawawezi kusema wewe ni Makamu Mwenyekiti wa CCM maana umakamu haunipi uhuru wa kupiga watu makofi halafu nikaondoka salama.
Alisisitiza CCM haina visasi na mtu, lakini atakayekosea hukamatwa na polisi kwa kuwa wamesomeshwa kukamata, vilevile wamesomeshwa kusema kosa hili ni kosa, “sio kila anayekamatwa huwa polisi wametumwa, sio kweli.”
Awali mfuasi wa Chadema wilayani Urambo, Shabani Warioba alitoa ombi kwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Wasira akidai amemsikia Mwenyekiti wa chama chake cha CHADEMA yuko ndani, hivyo anataka kujua amefanya kosa gani na kama amefanya kosa anaiomba serikali ya Chama Cha Mapinduzi imsamehe hata kama ana makosa.