9 views 4 mins 0 comments

TASAF YAONGEZA MAHUDHURIO KLINIKI,SHULE

In KITAIFA
March 14, 2025

Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA

Na Mwandishi Wetu
MFUKO wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), kupitia ruzuku wanayotoa kwa kaya masikini, imewezesha mahudhurio ya watoto kutoka kaya hizo kuongezeaka kwa asiimia sita.

Hayo yamesemwa na Mratibu wa Malipo ya Walengwa kwa Mtandao, Josephine Joseph alipokuwaakizungumza kaktika Kongamano la Wadau wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania, uliofanyika jijini Dodoma.

Kongamano hilo la siku moja limebeba dhima ya kuimarisha ushirikiano  endelevu wa wadau, ili kuboresha simulizi za vyombo vya habari kuchagiza maendeleo ya Taifa.

Josephine amesema TASAF ilianza mwanzoni mwa 2000 ambapo ilijikita kwenye ujenzi wa miundombinu ya elimu na afya, barabara, na baadaye kugundua kuwa wananchi wa kaya maskni wanashindwa kunufaika na miundombinu hiyo kutokana na umasikini uliokithiri.
Alisema TASAF ilianza kutoa ruzuku za msingi na za masharti ya watoto kuhudhurio kliniki na shule ili kuziwezesha kaya maskini kutumia huduma hizo.

Mratibu huyo amesema uamuzi wa kutoa ruzuku umekuwa na matokeo chanya kwa wanufaika wa TASAF hasa katika eneo la afya, elimu na kiuchumi ambapo pamoja na kuinua uchumi wa kaya, imeongeza mahudhurio ya watoto shuleni na kwenye huduma za afya..

“Ruzuku ambayo tunatoa kwa wanufaika wa TASAF imekuwa na matokeo chanya kwenye elimu, afya na kiuchumi, hivyo kutoa tafsiri sahihi ya maendeleo ya Taifa,” amesema.

Josephine amesema kupitia TASAF zaidi ya vikundi 68,000 vimeanzishwa nchini kote na kuwa na akiba ya Sh.bilioni 7.8 ambazo zinazunguka kwenye uchumi wa nchi ambapo kati ya hizo, walengwa wamekopeshana zaidi ya Sh 3 bilioni..

Amesema pia wameanzisha afua ya ajira kwa jamii inayonufaika na TASAF, hali ambayo itaongeza mchango kwenye uchumi wa nchi na jamii kwa ujumla.

Aidha, amesema pia TASAF imewezesha watoto wanaotoka familia maskini kupata mkopo kwa asilimia 100 jambo ambalo halikuwepo awali.

Mratibu huyo alisema kwa mujibu wa utafiti uliofanywa mwaka 2017 hadi 2018 na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), ulionesha bila uwepo wa TASAF umaskini ungeongezeka kwa asilimia 7 hadi 8.

“Pia tumeweza kuchochea kaya kuongezeka mapato na matumizi, hali ambayo itachochea ukuaji wa uchumi,” amesema.

Akichangia katika kongamano Mhariri Mkuu wa Nipashe Digital, Salome Kitomari amesema TASAF imeweka utaratibu nzuri wa kuifikia jamii kwa kushirikiana na vyombo vya habari.

“Tunaona mnyororo wa thamani kwa wanufaika wa TASAF kwamba si kupewa fedha tu bali kuwawezesha kubadilisha maisha yao na sasa wapo watoto wa maskini wamefikia ndoto zao za kusoma hadi vyuo vikuu,”amesema.

Aidha, amesema mchango wa vyombo vya habari kwenye maendeleo ya kiuchumi ni mkubwa na ndio maana vimekuwa mstari wa mbele kuibua masuala ya kijamii.

Mwenyekiti wa MISA- TAN, Edwin Soko, amesema matarajio yake Kongamano hilo liwepo kila mwaka kwa kujumuisha wadau na wanahabari ili kujadili masuala ya uchumi, siasa na kijamii kwa maslahi ya Taifa.

Soko amesema MISA TAN inatamani kuona kila mdau anaguswa na maendeleo ya nchi, kwa kuelewa msingi sahihi wa kushirikiana.

“Sisi MISA TAN tunaamini kwenye malumbano ya tija yenye hoja za kujenga Taifa hivyo tunawaomba wadau  kutambua MISA Wadau Summit kama jukwaa la majadiliano ya kimaendeleo na kuleta suluhisho,” amesema.

Amesema ushuhuda ulitolewa na TASAF katika kubadilisha maisha ya Watanzania unapaswa kujulikana kwa kila mtu na kupitia kongamano kama hili wananchi watajua.

/ Published posts: 1816

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram