15 views 4 mins 0 comments

MSAJILI WA HAZINA AMEZINDUA USHIRIKIANO KATI YA BENKI YA TAIFA YA BIASHARA TCB NA SOKO LA HISA DSE

In BIASHARA
February 21, 2025

Msajili wa Hazina Nehemia Mchechu amezindua ushirikiano kati ya Benki ya Taifa ya Biashara (TCB) na Soko la hisa la Dar es Salaam (DSE)

ambao unakwenda kutoa fursa kwa wateja wa benki hiyo kufanya miamala ya uwekezaji ya kuuza au kununua hisa kwa kutumia simu ya mkononi.

Akizungumza leo Februari 21, 2025 jijini Dar es Salaam wakati akizundua ushirikiano wa Benki ya TCB na DSE, Msajili wa Hazina Bw. Nehemia Mchechu, amesema kuwa ushirikiano huo ni mabadiliko makubwa kwa benki kwani itawasaidia watanzania wengi kujua umuhimu wa soko la hisa.

Mchechu amesema kuwa ushirikiano unakwenda kuogeza wigo wa kufanya uwekezaji na kutoa fursa kwa watanzania kuwa sehemu ya umiliki wa miradi mbalimbali.



“Soko la hisa ni sehemu muhimu kwa wafanya biashara na wawekezaji kukuza na kuongeza mitaji yao na kuleta manufaa makubwa katika uchumi” amesema Mchechu.

Mchechu amesema kuwa wakati umefika kwa wadau pamoja na mamlaka husika kuangalia namna ya kuongeza washiriki katika soko la hisa pamoja na kuleta mazao mbalimbali katika soko hilo.

Ameeleza kuwa wakati umefika kwa wafanyabishara kujua manufaa halisi ya soko la hisa kwa kuuza hisa zao kwani zinakwenda kuleta manufaa katika usimamizi wa uendeshaji wa makampuni hasa wanapokuwa na wana hisa wengi.



Mchechu amesema kuwa serikali ipo katika mpango wa kuleta taasisi nyingi katika soko la hisa, huku akieleza kuwa wanaendelea kufanya utafiti ili kujua taasisi gani iweze kuingia katika soko hilo.

“Tunaangalia ni taasisi ipi na muda gani inatakiwa kupelekwa katika soko la hisa, kwani kuna taasisi zaidi ya 248 na hatuwezi kuzipeleka zote, kwani lengo kupata matokeo chanya katika uwekezaji ” amesema Mchechu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya TCB Bw. Adam Mihayo, ameishukuru DSE kwa kuwapa fursa ya kuwa benki ya kwanza kuingia katika mashirikiano na kuwafanya kuwa benki kiongozi na kinara katika ubunifu wa kuja na bidhaa zinazoigusa jamii.



Mihayo amesema kuwa ushirikiano huo unakwenda kuwa saidia wateja wao kufanya miamala ya uwekezaji wa kuuza au kununua hisa kwa kutumia simu ya mkononi.

“TCB imekuwa benki ya kwanza kuja na huduma mbalimbali ikiwemo kutoa mkopo kwa wastaafu ambapo hadi sasa tumetoa shilingi trilioni moja, ushirikiano na makampuni ya simu kupitia ya huduma ya kikoba kiganjani na kufanikiwa uvifikia vikundi 500,000 pamoja na kushirikiana na SGR kwa kutumia mifumo yetu kukusanya fedha” amesema Mihayo.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es salaam (DSE) Bw. Peter Nalitolela, amesema kuwa ushirikiano huo unakwenda kutoa fursa kwa watanzania ambao wapo nje ya nchi kufanya uwekezaji.

“Wateja wa benki ya TCB watapata fursa ya kuwekeza katika soko la hisa na kuongeza ushiriki kwa watanzania katika soko hilo, DSE tunaendelea kufanya maboresho ili kuhakikisha watanzania wanawekeza bila kwenda katika Ofisi za mawakala wa soko” amesema Nalitolela.



Nae, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), CPA Nicodemus Mkama, ameipongeza benki ya TCB kuja na ubunifu ambao utakuwa na matokeo chanya katika masoko ya mitaji kwa sababu unaenda kuwavutoa Wawekezaji wengi kuna katika masoko ya mitaji.

CPA. Mkama amesema kuwa ili kufikia malengo wanaendelea kuweka mazingira wezeshi na shirikishi ili kuhakikisha wananchi wengi wanashiriki katika masoko ya mitaji.

“Kumeongezeka kwa imanai katika masoko ya mitaji nchini Tanzania kwani yapo imara na yanaendelea kukua na kuwa kivutio kikubwa kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, soko la mitaji kuna bidhaa nyingi ambazo zimeweka alama kubwa ulimwenguni ikiwemo kuwa hati fungani ya kwanza ya kijani” amesema CPA. Mkama.

/ Published posts: 1734

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram