22 views 3 mins 0 comments

TANZANIA NA MISRI KUSHIRIKIANA KUKUZA  SEKTA YA UTALII

In KITAIFA
February 19, 2025



Na Happiness Shayo- Dar es Salaam

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  na Jamhuri ya Kiarabu ya Misri,  zimekutana kujadiliana namna bora ya kushirikiana katika kukuza na kuendeleza utalii baina ya nchi hizo mbili.

Hayo yamejiri leo Februari 18,2025 jijini Dar es Salaam katika kikao kati ya  Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) na Balozi wa Misri nchini Tanzania, Mhe. Sherif Abdelhamid Ismail.

โ€œNchi zetu zinafurahia uhusiano wa kidiplomasia wa muda mrefu na wenye manufaa, ambao tunaamini unaweza kuwa ushirikiano thabiti katika Sekta ya  utalii piaโ€ Mhe. Chana amesisitiza huku akifafanua kuwa Tanzania inatamani kuongeza idadi ya watalii kutoka nchini Misri na kuvutia wawekezaji kuangalia fursa mbalimbali za utalii zinazopatikana nchini Tanzania.

โ€œTanzania ina fursa nyingi za uwekezaji katika mnyororo wa thamani wa mazao ya utalii ikijumuisha katika eneo la huduma ya malazi, usafirishaji, mashirika ya ndege, shughuli za utalii, vifaa vya mikutano,uwindaji wa kitalii na kisiwa kizuri katika Bahari ya Hindi, kinachofaa kabisa kwa uwekezajiโ€ alisema Mhe. Chana.

Alifafanua kuwa kwa mwaka 2023, Tanzania ilikaribisha watalii 9,517  tu kutoka nchini Misri hivyo ili kuongeza idadi ya watalii kutoka nchini humo, nchi hizo mbili zinapaswa kuweka kipaumbele katika kuimarisha ushirikiano kati ya mashirika yao yanayohusika na kukuza utalii ili kuboresha mabadilishano ya watalii kati ya mataifa hayo na kuanzisha programu za kubadilishana uzoefu kutasaidia kukuza utaalamu na mbinu bora katika kukuza utalii.


Kwa upande wake Balozi wa Misri nchini Tanzania, Mhe. Sherif Abdelhamid Ismail alisisitiza kuwa kwa wingi na upekee wa vivutio ilivyonavyo, Tanzania ina uwezo wa kuvutia zaidi ya watalii milioni 10 kwa mwaka, na ofisi yake iko tayari kushirikiana na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii katika kuendeleza na kutangaza utalii nchini.

Aidha, Balozi Ismail alisema kuwa anaridhishwa na ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Misri katika miradi mbalimbali na  kwamba yuko tayari kuendeleza ushirikiano katika Sekta ya Utalii hivyo ni muhimu kuwepo kwa hati ya makubaliano (MoU) itakayoainisha maeneo ya mashirikiano.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Watendaji kutoka Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT), Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Makumbusho ya Taifa la Tanzania (NMT), Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

/ Published posts: 1733

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram