17 views 2 mins 0 comments

NI KILWA TENA, MELI ZILIZOSHEHENI WATALII ZAPISHANA KUTIA NANGA

In KITAIFA
February 10, 2025



Na Beatus Maganja

Wahenga walisema isiyo kongwe haivushi, lakini leo Kilwa imetuvusha. Hayawi hayawi yamekuwa, leo Tanzania inathibitisha yale yaliyosemwa na wahenga miongo kadhaa pale mji wa kihistoria wenye historia ya kipevu mji wa Kilwa Mkoani Lindi unaposhuhudia mpishano wa meli kubwa za kifahari za Kitalii zilizosheheni watalii kutoka pembe za dunia zikishusha mamia ya watalii katika Hifadhi ya urithi wa utamaduni wa dunia ya Magofu ya Kale ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara.

Ilikuwa  Februari 09, 2025 majira ya  Saa 2 asubuhi katika bandari ya mji wa Kilwa wahifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania – TAWA na wakazi wa mji huo walipokusanyika kuwalaki wageni kutoka Mataifa mbalimbali duniani.

Taratibu Meli kubwa ya viwango vya Kimataifa ijulikanayo Kwa jina la Ponant Le Bougainville kutoka visiwa vya Seycheles yenye hadhi ya kutia nanga katika bandari ya nchi yenye utajiri wa vivutio vya utalii, nchi  inayoongozwa na Kiongozi shupavu mwenye maono Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ilianza kushusha watalii mmoja baada ya mwingine na kufikisha Idadi ya watalii 124.

Bendera za Mataifa takribani 14, zilionekana zikipepea Kilwa Kisiwani huku wanawake Kwa wanaume, watoto kwa wakubwa wakizuru sehemu mbalimbali za Hifadhi hiyo ya kihistoria yenye vivutio vingi vya asili na urithi wa kiutamaduni. Sura za wageni hao zikionekana kujaa bashasha na shauku ya kujifunza mengi huku majengo yaliyojengwa kwa ustadi wa ajabu yakichagiza udadisi wao.

Australia, ubeligiji, Canada, Ufaransa, Ujerumani, Ireland, Italia, Uholanzi na New Zealand ni miongoni mwa Mataifa yaliyotembelea Hifadhi hiyo bila kusahau Ureno, Shelisheli, Uswisi, Uingereza na Marekani.

Machweo yalipowadia watalii walianza kuingia ndani ya meli ya kifahari, na  taratibu Meli kuanza kutikia huku wageni hao wakipunga mikono yao Kwa Wakazi wa Kilwa na wahifadhi wa TAWA Hifadhi ya urithi wa utamaduni wa dunia Magofu ya Kale ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara.

Hii ni Meli ya 5 ya kitalii kutia nanga Kilwa tangu mwaka 2025 ulipoanza. Mpishano wa meli hizi kushusha watalii Kilwa ni kielelezo cha mapinduzi makubwa katika Sekta ya utalii na mabadiliko ya kiuchumi yaliyoletwa na Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

/ Published posts: 1712

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram