5 views 2 mins 0 comments

MGODI WA NDOLELA MWANGA MPYA KWA WANANCHI

In KITAIFA
February 05, 2025

Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA

_•       Waanza ujenzi wa Zahanati kuondoa kero kwa wananchi_

_•       Wasaidia upatikanaji wa urahisi wa kokoto katika marekebisho ya ujenzi wa barabara ya Iringa, Dodoma_



MGODI wa Mawe wa Ndolela Quarry uliopo kijiji cha Ndolela jimbo la Isimani mkoani Iringa umeanza ujenzi wa Zahanati kwa kushirikiana na wananchi ambayo itaondoa adha  ya  wananchi hao kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya.

Akizungumza katika mahojiano maalum, Mwenyekiti Mtendaji wa Kijiji cha Ndolela, Majuto Dumicus amesema Zahanati hiyo ikikamilika itaweza kuhudumia Kaya 377 zilizopo katika eneo hilo.


Amesema, ujenzi wa Zahanati hiyo ni kutimiza takwa la kisheria  na Kanuni za Wajibu wa Wamiliki wa Leseni za Madini Kwa Jamii.

Kwa upande wa Meneja Msaidizi wa Mgodi wa Mawe wa Ndolela (Ndolela Quarry) Hilter Ranjiti amesema tangu kuanzishwa kwa mgodi huo mwaka 2022 umekuwa na manufaa kwa wananchi kwa kutoa ajira pia kutekeleza takwa la kisheria kwa kuchangia miradi ya maendeleo.


“Mgodi huu umekuwa na faida kwa wakazi wa Iringa, miradi mbali mbali ya Serikali tumekuwa tukichangia, umerahisisha pia upatikanaji wa kokoto mkoani Iringa siku za nyuma walifuata Lugoba au Dodoma,”amesema Ranjiti.


Aidha amesema, mgodi huo upo kwenye  ujenzi wa Zahanati ya kijiji cha Ndolela na pia wamechangia marekebisho ya barabara ya Dodoma- Iringa.


Kwa upande wa mchimbaji mdogo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mgodi wa Madini ya Shaba Matembo, Elias Kazikuboma amesema mgodi huo mchanga umekuwa ukitoa huduma mbali mbali za kijamii kama ujenzi wa matundu ya vyoo pamoja na vifaa mbalimbali.


Amesema changamoto kubwa ipo kwenye vifaa vya uchimbaji ingawa soko la uhakika la madini ya shaba lipo.

Naye, Mwenyekiti wa Wachimbaji Mkoa wa Iringa ambaye pia ni miongoni mwa wamiliki wa mgodi wa Konga, uliopo kijiji cha  Itengulinyi, Ibrahim Msigwa amesema changamoto kubwa ya wachimbaji  wadogo ni mitaji.

“Tunawakaribisha wawekezaji wakubwa waje tushirikiane dhahabu zipo tushirikiane ili tuweze kuvuna,”amesema.

Aidha, amesema uwepo wa mgodi wa Itengulinyi wananchi wanafaidika kutokana na shughuli za maendeleo ikiwemo ujenzi wa nyumba ya daktari wa zahanati ya kijiji ambapo mgodi huo umechangia  tofali.

/ Published posts: 1701

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram