
Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Tuzo za za Kimataifa ya Kuhifadhi Quraan yatakayofanyika Aprili 23 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Aidha Taifa la Saudi Arabia, limetangaza neema katika mashindano hayo ikiwa ni pamoja na kumleta mmoja wa maimamu wakubwa wa msikiti mtakatifu wa Macca nchini humo na kutoa tiketi za hija kwa watu watano ambao watakuwa ni wageni wa Mfalme wa taifa hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam, jana,Mwenyekiti wa Taasisi ya Kuhifadhisha Quraan Tanzania ambao ni wandaaji wa tukio hilo, Sheikh Othuman Kapolo, alisema, washiriki katika mashindano hayo ni 25 kutoka mabara yote matano duniani.
“Awamu hii tutafanyia tukio hili katika Uwanja wa Benjamin Mkapa. Panapo maajaliwa mgeni Rasmi anatarajia kuwa Rais Dk. Samia,”alisema.
Alieleza, mashindano hayo awamu hii yatashirikisha makundi mawili ya watoto na vijana wa umri wa miaka kuanzia 17 na 25.
“Tunawashukuru wenzetu wa Saudi Arabia wamekubari kushiriki kikamilifu katika maandalizi na kufanikisha tukio lote la utoaji wa tuzo hizi. Wameahidi watatoa tiketi tano kwa wananchi watakaofika katika Uwanja wa Mkapa kwaajili ya kwenda Hija nchini humo,”alisema Sheikh Kapolo.
Alisema licha ya tiketi hizo pia kutakuwa na zawadi mbalimbali kwa wananchi watakaohudhuria zikiwemo simu na pikipiki, hivyo kuwahimiza wananchi kuhudhuria kwa wingi kwani hakutakuwa na kiingilio.
Alisema kwa washindi watakaoshindanishwa katika kuhifadhi Quraan tukufu watakabidhiwa tuzo za kimataifa ambapo pia tuzo mbalimbali za kitaifa zitatolewa.
Alisema ujumbe wa utoaji wa Tuzo za Kimataifa za Quraan mwaka huu usema Quraan ni amani.
“Pia ujumbe huu umezingatia mwaka huu ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu, hivyo amani tuliyonayo tunatakiwa kuilinda na Quraan ni amani,”alisema Sheikh Kapolo.
Awali Balozi wa Saudi Arabia hapa nchini , Yahya Ahmed Okeish, alisema tuzo za kimataifa za Quraan tukufu kama mbegu iliyopandwa na imechipua kwa watanzania.
” Fahari ya Mola katika Quraan ni kwamba yeye ndiye aliyeshusha Quraan na yeye ndiye anayeitunza Quraan ispotee. Lakini cha kushukuru katika maeneo mbalimbali duniani kuna ambao wamejitolea kuisimamia kupitia vijana mbalimbali kwa kuwahifadhisha.
Miongoni mwao ni Sheikh Othuman Kapolo,” alisema Balozi Okeish.
Alisema, mwongoni mwa bipaumbele vya Mfalme wa SaudiArabia ni kuwahudumia watu wa Quraan.
Katika Mji Mtakatifu wa Madina kuna kiwanda kinacho chapisha misahafu katika mifumo mbalimbali, ikiwemo ya kusoma, sauti na kwa wasioona hivyo taifa hilo linanafasi kubwa ya kuhakikisha usomaji wa Quraan unasonga mbele.
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega ambaye ni Mbunge wa Mkuranga, yalipo makao makuu ya Taasisi ya Kuhifadhisha Quraan Tukufu Tanzania, aliwataka wananchi kuhidhuria kwa wingi katika masgindano hayo muhimu.
Ulega alisema ujumbe wa mwaka huu wa Quraan ni amani ambao ni muhimu hasa wakati huu ambapo taifa linaelekea katika uchaguzi mkuu.
Alisema Rais Dk. Samia, amelekeza wasaidizi wake yapofika mambo mema hasa ya kidini ni kuyapa kipaumbele.
Awali akizungumza kwa niaba ya Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zubeir, Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Walid Alhad, aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kuhudhuria tukio hilo muhimu.
“Jambo hili lionekane linasimasishwa kwa hadhi ya Rais na hadhi ya Quraan,”alisema Sheikh Alhad.