Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA
MOROGORO-Uongozi wa Chama cha Wafanyakazi (TUGHE) tawi la Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) umepongezwa kwa kusimamia vyema maslahi ya wafanyakazi, hali iliyosaidia kupunguza malalamiko yao kwa kiwango kikubwa.
Pongezi hizo zimetolewa na Meneja wa Utawala na Rasilimali Watu wa TFRA, Naomi Fwemula, aliyemwakilisha Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi, Victoria Elangwa wakati wa hafla ya kufunga mafunzo ya wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa mamlaka hiyo yaliyofanyika katika Ukumbi wa Morena, Morogoro.
“TUGHE imesaidia sana katika kusimamia haki za wafanyakazi na kuishauri menejimenti kuhusu mbinu bora za kutatua changamoto za watumishi,”amesema Fwemula.
Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wajumbe wa baraza na menejimenti kuelekea kikao cha Baraza la Wafanyakazi la TFRA ili kujua wajibu wao pindi wanaposhiriki vikao hivyo.
Kamishna Msaidizi wa Kazi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Andrew Mwalwisi, aliwaasa watumishi hao kuheshimu sheria, kanuni, na miongozo ya utumishi wa umma ili kuepuka migogoro isiyo ya lazima eneo la kazi.
Katika mada yake kuhusu Haki na Wajibu wa Watumishi wa Umma, Mwalwisi alisisitiza kuwa kanuni za utumishi ndizo zinazoeleza haki za mtumishi, hivyo ni jukumu la kila mfanyakazi kuzizingatia ili kuepuka mgongano na waajiri wao.
Mafunzo hayo yalihusisha mada mbalimbali, zikiwemo mabadiliko ya mtazamo (attitude change), majukumu ya wajumbe wa baraza, na uandaaji wa hoja za wafanyakazi na Haki na Wajibu katika Utumishi wa Umma.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi (TUGHE) TFRA, Aziz Mtambo, amewasihi watumishi wa Mamlaka kujiunga na chama cha wafanyakazi ili waweze kunufaika na huduma zinazotolewa na chama hicho lakini pia itasaidia uundaji wa Mkataba wa Hali bora utakosaidia kusimamia maslahi ya wafanyakazi.
Alibainisha kuwa, kwa sasa ni watumishi 34 pekee kati ya 89 wa TFRA waliojiunga na TUGHE, lakini idadi hiyo imeongezeka kutoka 12 waliokuwepo mwaka wa 2021/2022.
Mtambo pia ameishukuru Menejimenti kwa kushughulikia zaidi ya asilimia 70 ya hoja zilizowasilishwa katika kikao cha mwaka 2023/2024, akisema hatua hiyo inaonyesha ushirikiano mzuri kati ya menejimenti na chama cha wafanyakazi.