12 views 2 mins 0 comments

TFRA YATOA ELIMU YA MBOLEA KWA VITENDO KUPITIA MASHAMBA DARASA MIKOA YA LINDI NA MTWARA

In BIASHARA
January 21, 2025

Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kwa kushirikiana na kampuni za mbolea za ETG na Itracom zimefanikiwa kusambaza tani nne za mbolea kwa ajili ya kutoa elimu kwa vitendo kupitia mashamba ya mfano yaliyoanzishwa katika Halmashauri zote za mikoa ya Lindi na Mtwara.

Elimu hiyo inalenga kuwahamasisha wakulima kutumia mbolea kwenye shughuli zao za ili kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao ya chakula na hivyo kukuza Uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Hadi kufikia Januari 2025, mafunzo kwa vitendo yamefanyika katika Halmashauri za Mtwara Vijijini, Newala, Masasi DC, Masasi TC, Ruangwa, Mtama, Lindi MC, na Kilwa.

Mashamba hayo ya mfano yanawawezesha wakulima kujifunza matumizi sahihi ya mbolea na mbinu bora za kilimo, hatua inayolenga kuongeza uelewa wa kilimo kinachozingatia kanuni bora za kilimo kunakopelekea kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula katika mikoa hiyo.

Akizungumza kuhusu utekelezaji wa mpango huo, Afisa Kilimo Mwandamizi wa Mkoa wa Mtwara, Bw. Ali Linjenje, alisema kuwa, mkoa wake umelenga kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula kutoka tani 433,000 msimu wa 2023/2024 hadi kufikia tani 616,000 msimu wa 2024/2025.

Aliongeza kuwa, hamasa kubwa inahitajika kwa wakulima, hasa katika matumizi ya mbolea, ili kufanikisha lengo hilo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mtwara Vijijini, Bw. Abeid Kafunda, aliahidi kushirikiana kwa karibu na TFRA katika kuhamasisha matumizi sahihi ya mbolea kupitia mashamba ya mfano.

Bw. Kafunda alisema, ni aibu kwa Mkoa wa Mtwara kutegemea chakula kama mchele kutoka mikoa jirani kama Morogoro na Pwani, ilhali tuna ardhi nzuri inayofaa kwa uzalishaji wa mazao ya chakula.

Naye, Afisa Udhibiti Ubora Mwandamizi wa TFRA, Bw. Swalehe Mkuwili, alisisitiza kuwa, TFRA itaendelea kushirikiana na Halmashauri zote za mikoa ya Lindi na Mtwara ili kuhakikisha wakulima wanapata elimu ya matumizi sahihi ya mbolea moja kwa moja kupitia mashamba ya mfano.

Hatua hii iliyochukuliwa na Mamlaka  ni utekelezaji ya maelekezo ya Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Hussein Bashe, aliyoyatoa Oktoba 2, 2024, wakati wa ziara yake mikoa ya Lindi na Mtwara.

Waziri alihimiza TFRA kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa na kampuni za mbolea ili kuongeza kasi ya matumizi ya mbolea na kuhakikisha uzalishaji wa mazao ya chakula unaongezeka katika mikoa hiyo.

/ Published posts: 1657

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram