15 views 2 mins 0 comments

TFRA YAENDELEA KUHAMASISHA MATUMIZI SAHIHI YA MBOLEA MKOANI KAGERA

In BIASHARA
December 25, 2024

Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imeendelea kuchukua hatua za kuelimisha wakulima kuhusu matumizi sahihi ya mbolea na faida zake kupitia ushiriki wake katika maadhimisho ya “Ijuka Omuka” yanayoendelea katika viwanja vya CCM mjini Bukoba. Maadhimisho haya, ambayo yalianza tarehe 16 Desemba 2024, yamelenga kuwakutanisha wadau wa maendeleo katika Sekta ya kilimo, biashara, na jamii kwa ujumla.

Katika banda la TFRA, wakulima wanapata fursa ya kujifunza mbinu bora za kilimo kupitia matumizi sahihi ya mbolea.             Aidha, Mamlaka inaendelea kuhamasisha wakulima kujisajili kwenye mfumo wa ruzuku ya mbolea unaosimamiwa na Mamlaka hiyo hatua inayowahakikishia wakulima fursa za kupata mbolea na mbegu kwa gharama nafuu.

Meneja wa Kanda ya Ziwa, Bw. Michael Sanga, amesema kuwa lengo kuu la ushiriki wa Mamlaka  ni kuhakikisha wakulima wanajua umuhimu wa matumizi sahihi ya mbolea, ambayo yanaongeza virutubishi kwenye udongo na kuboresha mazao.

Ameongeza kuwa, ni muhimu wakulima kufuata kanuni za matumizi ya mbolea: kuweka mbolea sahihi, kwa kiasi sahihi, katika muda sahihi, na kwenye sehemu sahihi.

Pamoja na hayo, Bw. Sanga amewasihi wakulima kuachana na imani potofu kuwa mbolea za viwandani zinaharibu udongo.

Alisisitiza kuwa mbolea hizi, zinapotumika ipasavyo, huchangia kuongeza uzalishaji wa mazao na kuimarisha uchumi wa mkulima.

Wakulima waliotembelea banda la TFRA wamefurahia elimu na huduma zinazotolewa, huku wakipewa fursa ya kujiandikisha kwenye mfumo wa ruzuku. Wananchi wa Kagera wametakiwa kutumia nafasi hii adimu kutembelea banda hilo, kujifunza, na kufaidika na huduma zinazotolewa.

Maadhimisho ya “Ijuka Omuka” yanatarajiwa kuendelea hadi tarehe 1 Januari 2025, huku TFRA ikisisitiza dhamira yake ya kuendeleza kilimo chenye tija na kuimarisha maisha ya wakulima nchini.

/ Published posts: 1606

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram