19 views 4 mins 0 comments

UJENZI WA KIVUKO CHA TRIPPI KUPUNGUZA UTORO KWA ASILIMIA 98 – MBULU

In KITAIFA
December 13, 2024

Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA

Ahadi ya Rais yatekelezwa

Kukamilika kwa ujenzi wa kivuko cha mto Trippi kilichopo Kijiji cha Trippi Kata ya Gehandu Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu umeweza kupunguza utoro kwa asilimia 98 na kuongeza ufaulu wa mtihani wa darasa la saba kwa asilimia 91 kwa wanafunzi wanaosoma Shule ya Msingi Trippi.

Hayo yameelezwa na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Trippi Mwl. Adwee Hesiali ambapo amesema kabla ya kivuko hicho wanafunzi wanaoishi upande wa pili walikuwa wakikosa masomo kwa takriban miezi minne na kipindi cha masika ilifika hadi asilimia 51.

“Wananchi walijitahidi kujenga kivuko cha miti lakini kilisombwa na maji kwenye mto huu, lakini kukamilika kwake kimeweza kuongeza ufaulu kutoka asilimia 84 mwaka jana hadi kufikia asilimia 91 mwaka huu.

“Kwa kweli kitaaluma tumepanda na utoro umekwisha, hii ni kutokana na ujenzi wa kivuko hiki kwani imetuondolea adha kwa wanafunzi wetu”.

Mwl. Hesiali amesema kuwa wanaishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha kivuko hiko na kuongeza kusema kwamba kwa sasa wapo vizuri.

Naye, Diwani wa Kata ya Gehando Mhe. Alex Tango ameishukuru Serikali kupitia TARURA kwa kuwajengea kivuko katika mto Trippi “Kivuko hiki  kimekuwa mkombozi kwa wanafunzi ambao walishindwa kuhudhuria masomo katika kipindi chote cha masika”.

Amesema kivuko hicho imesaidia pia kuinua uchumi wa wananchi kwa upande wa pili kwani kuna wakulima wa mbaazi ambao walikuwa wanavusha  mizigo kwa kichwa ila kwa sasa hawana shida tena na kusema msimu ujao wanatarajia kivuko hicho kitasaidia sana kuinua kipato cha wananchi wake.

Mhe. Tango alisema licha ya ujenzi wa kivuko hiko, TARURA hivi sasa kuna kazi ya ujenzi wa barabara ya Kainamu-Hasama- Tsawa yenye urefu wa Km. 10 ambapo ujenzi wake utagharimu shilingi milioni 700 ambapo kukamilika kwake kutasaidia wakazi zaidi ya 14,000.

“Kwakweli mimi kama mwakilishi wa wananchi naipongeza sana Serikali kwa kazi kubwa hii wanayoifanya kilomita hizi za barabara  zikikamilika wananchi watakuwa wamepata mawasiliano na hivyo kujenga imani na Serikali yetu”.

Amesema wameweka mkakati wa kutunza kivuko hicho kwa kuzungumza na viongozi wa Kijiji na Kata na hivyo kuweka utaratibu wa kuvusha mizigo mikubwa kwa kuweka ulinzi ambao utasaidia kulinda wizi wa vyuma.

Kwa upande wake Bw.Silini Esumale mkazi wa kijiji cha Tsawa ameishukuru Serikali kwa kuwajengea kivuko cha utalii kwani miaka yote watoto wao hawakuwa wakipata masomo pia wakazi wengi walikuwa wakipata matatizo mengi, lakini kilio chao cha muda mrefu Serikali imekisikia na sasa wanapita bila wasiwasi.

Meneja wa TARURA Wilaya ya Mbulu Mhandisi Nuru Hondo amesema kwamba katika Halmashauri ya Mji wa  Mbulu na Halmashauri ya wilaya wameweza kutekeleza ahadi ya Mhe. Rais kwa kujenga barabara ya lami yenye urefu wa Km. 11.2 katika Mji wa Mbulu (4.2),Mji wa Dongubesh (2.5) na Mji wa Haydom (4.4).

Amesema katika kipindi cha miaka mitatu bajeti ya wilaya imeweza kuongezeka kwa 42.1%  hadi kufikia shilingi bilioni 7.59 kwa mwaka 2023/2024 ukilinganisha na shilingi bilioni 4.41 mwaka 2021/2022, ambapo wameweza kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo madaraja 22 (Mbulu), madaraja 17 (Mbulu Mji)  na hivyo kuweza  kuhudumia mtandao wa barabara wa Km. 1,500.459.

/ Published posts: 1606

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram