28 views 2 mins 0 comments

UWEKEZAJI SEKTA YA NISHATI TANZANIA KUNUFAISHA NCHI WANACHAMA EAPP – MHE.KAPINGA

In KITAIFA
December 10, 2024

Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA

Ashiriki Mkutano wa Nchi Wanachama wa EAPP nchini Kenya*

Aeleza jinsi Tanzania inavyotekeleza miradi ya umeme kwa ufanisi*

Asema zaidi ya asilimia 99 ya Vijiji nchini vimesambaziwa umeme*

Naibu Waziri Nishati, Mhe. Judidhi Kapinga amesema uwekezaji uliofanyika kwenye Sekta ya nishati nchini Tanzania  katika kipindi cha miaka mitatu itazinufaisha Nchi Wanachama wa Umoja wa Mashariki mwa Afrika (EAPP) katika biashara ya kuuziana na kununua umeme.

Mhe. Kapinga ameyasema hayo leo Desemba 09, 2024 Mombasa nchini Kenya katika  mkutano uliowakutanisha nchi wanachama wa EAPP na wadau mbalimbali katika sekta ndogo ya umeme.

“Uzalishaji wa umeme awali ulikuwa kwa kiasi kikubwa ukitegemea gesi, lakini baada ya ujenzi wa mradi mkubwa wa Julius Nyerere ambao kwa sasa unazalisha takribani megawati 1,175 tumekuwa tukitumia zaidi nishati ya maji kuzalisha umeme.” Amesema Mhe. Kapinga

Ameongeza kuwa, Tanzania inazingatia suala la uzalishaji wa umeme kwa nishati mchanganyiko (energy mix) na kutoa wito kwa Nchi wanachama EAPP kuwekeza zaidi katika nishati jadidifu ambazo ni nishati safi.

Kuhusu usambazaji wa umeme Vijijini, Mhe. Kapinga ameeleza kuwa Tanzania ina mkakati wa kuhakikisha Vijiji vyote 12,318 vinafikiwa na nishati ya umeme ifikapo 2025 na kuongeza kuwa tayari zaidi ya  asilimia 99 ya vijiji vimeshafikiwa na nishati hiyo.

Kapinga ameeleza kuwa, Tanzania inatarajia kujiunga na mfumo wa kuuziana na kununua umeme wa Kusini mwa Afirka (Southern African Power Pool).

Amesisitiza kuwa, kwa Tanzania kuwa na miunganiko ya umeme ni muhimu na ndio maana kama  inaungana na nchi tofauti tofauti katika biashara ya umeme ili kuufanya mfumo wa gridi kuwa imara.

Kapinga amesisitiza kuwa Nchi nyingine za Afrika zitanufaika na sekta ya nishati kutokana na uwekezaji unaoendelea kufanyika nchini kwa uwepo wa umeme wa uhakika.

Kwa upande wa Wadau wa Maendeleo, Mhe. Kapinga ameeleza kuwa Tanzania inathamini mchango wao katika sekta sekta ya nishati na kuongeza kuwa kwa kiasi kikubwa miradi inatekelezwa kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo.

/ Published posts: 1588

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram