Na Kassim Nyaki, NCAA.
Zoezi la kunadi vivutio vya utalii vilivyopo eneo la hifadhi ya Ngorongoro kuelekea msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka limefika Zanzibar ambapo kampeni hiyo imepokelewa kwa kishindo, shangwe na bashasha kwa wananchi wa Zanzibar.
Meneja wa Idara ya huduma za Utalii na Masoko NCAA, Mariam Kobelo ameeleza kuwa Zanzibar ni soko kubwa la kimkakati katika sekta ya utalii na watalii wengi wanaotembelea Zanzibar huunganisha safari zao kwenda Ngorongoro, hivyo ziara hiyo imepanua wigo wa kuwafikia ili kutangaza zaidi vivutio vya utalii vilivyopo, shughuli za uhifadhi na fursa za uwekezaji zilizopo.
“Watalii wanaokuja Zanzibar wakimaliza kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo wengi wao wanaunganisha safari kwenda Ngorongoro na Maeneo mengine, kwetu Zanzibar ni soko la kimkakati na katika kampeni yetu ya kuhamasisha utalii kuelekea msimu huu wa sikukuu pamoja na kupita mikoa mbalimbali lakini hapa Zanzibar muitikio umekuwa mkubwa na tumeungwa mkono na wananchi wengi ambao wameahidi kutembelea hifadhi ya Ngorongoro” amebainisha Kobelo.
Katika utekelezaji wa kampeni ya kutangaza utalii, NCAA imewatumia vijana maarufu wa _Makachu Jumpers_ katika eneo la Forodhani pamoja na kugawa vipeperushi katika mitaa mbalimbali ya Zanzibar ili kufikisha ujumbe kwa haraka zaidi hasa kuelezea vifurushi vya utalii kuelekea msimu huu wa sikukuu.
Vifurushi katika msimu wa sikukuu vimegawanyika katika aina tatu, Kifurushi cha kwanza ni FARU chenye gharama ya Shilingi 450,000, wanaolipia kifurushi hiki watafanya utalii kwa siku mbili (02) katika hifadhi ya Ngorongoro na gharama hizo zitajumuisha kiingilio, Malazi, Chakula, muongoza watalii, Usafiri na huduma ya picha ambapo watakaolipia kifurushi hicho safari ya Ngorongoro itafanyika tarehe 24-25 Desembaa 2024.
Kifurushi cha Pili ni TEMBO chenye gharama ya Shilingi 130,000 kwa mtu, kifurushi hiki kinahusisha utalii kwa siku moja (01) na gharama hiyo inajumuisha kiingilio, Chakula, muongoza watalii, Usafiri na huduma ya picha ambapo safari ya Ngorongoro itakuwa tarehe 25 Desemba, 2024.
Kifurushi cha tatu kinaitwa CHUI chenye gharama ya shilingi 85,000 kwa mtu na gharama hiyo itajumuisha Usafiri wa basi, kiingilio, Chakula, muongoza watalii, huduma ya picha na safari ya Ngorongoro itafanyika tarehe 29 Desemba, 2024.
Kwa upande wake kaimu meneja uhusiano wa NCAA Hamis Dambaya ameeleza kuwa kampeni hiyo tangu ilipozinduliwa Jijini Arusha tarehe 4 Desemba 2024 imeendelea kuwa na muitikio mkubwa ambapo wananchi wengi wameendelea kulipia vifurushi mbalimbali kwa ajili ya kwenda kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo Ngorongoro.
“Tangu tumeanza kampeni yetu tumeona mafanikio makubwa, tumekutana na wananchi mbalimbali kuwaelimisha kuhusu vifurushi vyetu, maeneo yote tuliyopita ikiwepo hapa Zanzibar tunafanya ziara katika vyombo vya habari kuelezea shughuli mbalimbali za uhifadhi, utalii na maendeleo ya jamii zinazofanyika hifadhi ya Ngorongoro ili kuendelea kuongeza uelewa kwa wananchi” alifafanua Dambaya.
Dambaya ameongeza kuwa katika msimu huu wa sikukuu za mwisho wa mwaka wananchi ambao wangependa kutumia ofa hiyo kutembelea Ngorongoro wanaweza kuchagua kifurushi chochote kati ya vitatu vilivyotangazwa kwa kupiga namba za simu 0755 559013 ili kuweka nafasi (booking).