32 views 6 mins 0 comments

RAIS SAMIA AWAPA NENO WENZA WA MARAIS AFRIKA

In KITAIFA
October 30, 2024

Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA

-DAR E SALAAM

RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka wake wa marais  Afrika kutambua kuwa wana nafasi muhimu kwa jamii na kuwaomba wabebe suala la nishati safi ya kupikia kwa hekima na kwa ushawishi mkubwa kwa marais.

Pamoja na hali hiyo amewataka waendelee kutoa ushauri wa hekima  katika kuangalia namna ya kuweka vipaumbele  vya afua vitakavyosaidia kuwawezesha wanawake na kuboresha ustawi wao.



Hayo aliyasema jana jijini Dar es Salaam katika ufunguzi wa mkutano wa 11 wa Taasisi  ya Merck Foundation  ambao umehudhuriwa na baadhi ya wake wa marais kutoka nchi 15 za Afrika na washiriki zaidi ya 400.

Kuokana na hali hiyo, Rais Samia alisema amekuwa akitumia nafasi yake katika  kuonesha mitazamo  iliyokosekana na  kutoa mapendekezo kwa lengo la kumkomboa mwanamke.

“Nyakati zote nimekuwa nikitumia nafasi yangu kuonesha mitazamo inayokosekana na kutoa mapendekezo ambayo yataweza kushughulikia masuala ya wanawake.

“Nimekuwa nikishughulikia suala la kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia katika Afrika ikiwa sehemu ya kuongeza usawa wa kijinsia katika kutumia nishati safi na kuachana na mkaa na kuni ambayo inaathiri afya za wanawake na ustawi wao na kuharibu mazingira,” alisema.

Licha ya hali hiyo alisema kuwa wamepokea msaada mkubwa wa kutekeleza mpango huo  ambao utawezesha wanawake na kuboresha ustawi wao katika Bara zima la Afrika.

“Nimefanya hayo kama Rais lakini leo (jana) niwakumbushe wake za marais kuwa mnayo nafasi muhimu katika jamii zenu, chukueni suala la nishati safi ya kupikia kwa hekima na kuwa na ushawishi mkubwa marais waichukue hiyo kama ajenda yao na kuwasaidia wanawake kutumia nishati safi ya kupikia,”alisema

Aidha aliwapongeza kwa kuwa na program za kufikia malengo ya hatima ya kuwa na watu wenye afya bora hasa wasichana na waanawake Afrika hivyo aliwataka waendelee kutoa ushauri kwa hekima katika kuangalia namna ya kuweka vipaumbele vya afua vitakavyosaidia  wanawake na kuboresha  ustawi wao katika nchi zao.

Mkuu huyo wa nchi, alisema kuwa Tanzania inayodhamira ya kuendelea  kushirikiana na washirika waliopo nchini kufikia hatma yenye afya na furaha zaidi kwa vizazi vijavyo.

“Tunathamini sana ushirikiano huu, umetuwezesha  Watanzania kupata mafunzo ya muda mfupi na mrefu ya ubobezi katika afya ni mategemeo yetu tutakuza ushirikiano huu katika miaka ijayo,” alisema.

Alisema miaka tisa iliyopita Umoja wa Mataifa uliopitisha  malengo 17 ya maendeleo endelevu SDGs, miongoni  mwa malengo hayo ni kuhakikisha kunakuwepo na elimu jumuishi, kuimarisha nyenzo za utekelezaji  wa ushirikiano wa kidunia kwa maendeleo endelevu.



Alipongeza kongamano hilo la 11 kwani limekuja wakati muafaka  ikiwa ni kipindi cha utekelezaji wa taarifa za maendeleo endelevu  hususani kwa sekta ya afya na elimu.

SEKTA YA AFYA

Akizumgumza katika mkutano huo, Rais Samia  alisema Serikali  yake imetoa kipaumbele kikubwa katika kuboresha afya mama na mtoto kwa kuongeza upatikanaji wa huduma za afya kwa kujenga hospitali za wilaya 127  na vituo vya afya 300.

“Tuliongeza idadi ya vituo vya kutolea huduma za afya ambavyo vinatoa huduma za uzazi na mtoto kutoka vituo 340 mwaka 2021 hadi 523, mwaka 2023, kupunguza vifo vya uzazi mwaka 2021 kutoka 556 kwa kila vizazi hai 100,000 hadi 104 ikiwa punguzo la zaidi ya asilimia 80,” alisema.

Rais Samia alisema vifo vya watoto vimepungua kutoka 67 hadi 43 kwa kila vizazi hai 1000 sawa na theluthi moja.

Alisema kuna hatua zaidi za kufanya kufikia malengo ya afya  ya mama na mtoto kwa kuendelea kuwekeza katika huduma za kibobezi kwa sababu moja ya changamoto wanayokumbana nayo ni upungufu wa wataalamu bobezi na wenye ujuzi.

SEKTA YA ELIMU

Rais Samia alisema elimu ni chanzo cha kumuwezesha mwanamke kufikia mafanikio makubwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo ya kiuongozi.

Alisema kwa Tanzania elimu imeendelea kuwa kipaumbele kwa  serikali kwani imechukua afua mbalimbali kwa sekta hiyo kwani kwa miaka mitatu iliyopita wamejenga zaidi ya shule 500 nchini.

DKT. GWAJIMA

Naye Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dkt. Dorothy Gwajima alisema mkutano huo ni wa kwanza kihistoria kufanyika nchini.

Alitaja vitu vilivyochangia mkutano huo kufanyika nchini ni ushirikiano wa Rais Samia na taasisi ya Merck katika jitihada za kukabiliana na matatizo na changamoto za kiafya na kijamii zinazoathiri jamii zetu hususani wanawake na wasichana.

Dkt. Gwajima alisema jamii kuelewa kukabiliana na changamoto hizo ni muhimu hasa wanapoendelea kuboresha upatikanaji wa huduma za afya na mijadala itakayowasilishwa haitashughulikia matatizo ya afya tu bali itahusu ku boresha maisha na kuunda mustakabali endelevu kwa jamii.

Alisema Tanzania imeweka mazingira mazuri ya kisera na kisheria katika  kukuza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake na wasichana nchini.

PROFESA HAVERKAMP

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa taasisi ya Merck, Profesa Frank Haverkamp alisema  taasisi hiyo  imejikita  katika kuboresha  Afya na ustawi  katika huduma za afya eneo la Afrika, Asia na kwingineko.

Haverkamp alisema katika kufanikisha jambo hilo, wamekuwa wakitoa udhamini wa masomo katika kada ya afya kwa ngazi tofauti na kutoa semina  kuhusu afya bora na ustawi wa afya.

/ Published posts: 1487

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram