41 views 3 mins 0 comments

TAWA YAWASILISHA TAARIFA YA UTENDAJI WAKE KWA KAMATI YA BUNGE

In KITAIFA
October 25, 2024

Na Beatus Maganja WAMACHINGA

Yapewa kongole Kwa Kasi ya ukusanyaji maduhuli, Utatuzi wa migogoro ya mipaka

Dodoma

Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania – TAWA leo Oktoba 24, 2024 katika ukumbi  namba 44 jengo dogo la utawala bungeni Dodoma imewasilisha taarifa ya utendaji wake ya mwaka 2023/24 kwa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii iliyojikita katika kudadavua majukumu ya kiuhifadhi na utalii katika kipindi husika.

Akiwasilisha taarifa hiyo mbele ya Mwenyekiti wa Kamati Mhe. Timotheo Mnzava (Mb) Kwa niaba ya Kamishna wa uhifadhi wa TAWA, Kaimu Naibu Kamishna wa Uhifadhi Mlage Kabange amesema katika kipindi cha mwaka 2024/25, Mamlaka imepanga kukusanya kiasi cha zaidi ya shilingi billioni 94 ambapo hadi kufikia mwezi Septemba, 2024 Mamlaka imekusanya zaidi ya shilingi bilioni 23.8 sawa na asilimia 102.96 ya lengo la robo ya kwanza ya mwaka.

Kuhusu ongezeko la matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu nchini Kabange amesema Wizara imekuja na mkakati wa kuvuna baadhi ya spishi za wanyamapori hao ili kupunguza athari Kwa maisha ya wananchi na mali zao ambapo amebainisha kuwa wanyamapori watakaovunwa ni mamba na viboko  katika maeneo  mbalimbali nchini yenye changamoto ya wanyama hao ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vizimba 10.

Sambamba na hilo, Mamlaka itaendeleza matumizi ya teknolojia ikiwemo kufunga visukuma mawimbi Kwa makundi ya tembo kwa ajili ya kurahisisha ufuatiliaji na matumizi ya mabomu baridi ambayo yameonekana kuleta matokeo mazuri kwa maeneo mbalimbali nchini.

Akiongelea suala la utatuzi wa migogoro ya mipaka, Mlage Kabange amesema Mamlaka imefanikiwa kuweka alama za mipaka za kudumu (vigingi) 826 katika Mapori ya Akiba manne (4) ambayo ni Kilombero, Mpanga/Kipengere, Liparamba na Igombe na Pori Tengefu Lunda Nkwambi hii ikiwa ni baada ya kushirikisha wananchi, Wizara za Ardhi na TAMISEMI na KU za Mikoa na Wilaya.

Vilevile Mamlaka imefanikiwa kulipa fidia ya Shilingi millioni 482.57 kwa wananchi wa maeneo  ya Kagera, Msumbiji na Elbebek yaliyopo katika Kijiji cha Kisondoko na eneo la Ndaja katika Kijiji cha Keikei Wilaya ya Kondoa katika Pori la Akiba Mkungunero ili waweze kuhama ndani ya hifadhi hiyo ili kupisha shughuli za kiuhifadhi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Mhe. Timotheo Mnzava ameipongeza TAWA Kwa kasi ya ukusanyaji maduhuli na kuitaka iongeze kasi ya kutangaza vitalu vya uwindaji wa kitalii.

Pia ameiomba Wizara iangalie namna ya kutatua changamoto ya uhaba/uchache wa watumishi wa TAWA ili kuongeza tija na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.

/ Published posts: 1480

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram