109 views 4 mins 0 comments

KONGAMANO LA KIMATAIFA LA JOTOARDHI LAANZA KWA MAFANIKIO DAR ES SALAAM

In KITAIFA
October 21, 2024

Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA

Lahusisha nchi 21 na Washiriki 800*

Kuangazia Sera, fursa za masoko na uwekezaji*

Kamishna Luoga asema lengo ni kuendeleza nishati ya Jotoardhi nchini*

UNEP yaipongeza Tanzania kwa maandalizi*

Kongamano la 10 la Jotoardhi Afrika (ARGeo-C10) limeanza kwa mafanikio jijini Dar es Salaam ambapo Wataalam takriban 800 kutoka 21 duniani wameshiriki.



Hayo yameelezwa na Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga wakati akifungua mafunzo kuhusu masuala mbalimbali ya Jotoardhi kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt. Khatibu Kazungu ikiwa ni sehemu ya programu ya siku saba za Kongamano hilo.

“Katika Kongamano hili washiriki watafaidika na masuala mbalimbali ikiwemo kupata ufahamu wa kina kuhusu maendeleo ya rasilimali za jotoardhi kupitia mazungumzo na warsha za kiufundi, Kubadilishana uzoefu, kutembelea na kujifunza kwa vitendo katika maeneo ya miradi ya jotoardhi, kujadili athari za masoko ya kaboni (carbon markets) na kukuza Uwezo kupitia kozi fupi za kiufundi (Pannel and Parallel Sessions).” Amesema Mhandisi Luoga



Ameongeza kuwa, Tanzania imekuwa mwenyeji wa kongamano hilo kutokana na juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika uendelezaji wa Sekta ya Nishati ikiwemo Jotoardhi.

“ Ili tuweze kuwa na umeme wa uhakika na usalama wa nishati nchini lazima umeme uzalishwe kutoka vyanzo mbalimbali ikiwemo Maji, Gesi, Jua, Upepo na Jotoardhi yenyewe na lengo la Serikali ni kuachana na utegemezi vyanzo vichache vya umeme.” Amesema Mhandisi Luoga



Ametanabaisha kuwa, Tanzania ina maeneo takriban 52 yaliyoainishwa kwa ajili ya uendelezaji wa  nishati ya Jotoardhi ambapo maeneo matano tayari yanaendelezwa, ikiwemo Ngozi, Kiejo-Mbaka, Ruhoi, Natron na Songwe.

Ameeleza kuwa, Kongamano hilo la Kimataifa la Jotoardhi linaamsha ari mpya katika uendelezaji wa Jotoardhi Tanzania kwani litasaidia pia kuongeza fursa za uwekezaji kwenye sekta hiyo.



Amesema Kongamano la ARGeo- C10 litafunguliwa na Makamu wa Rais, Mhe.Dkt.Philip Isdor Mpango ambapo nchi mbalimbali duniani zinazoshirikiana na Tanzania katika kuendeleza rasilimali ya Jotoardhi zinashiriki.

Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi Tanzania (TGDC), Mathew Mwangomba amesema Kongamano hilo linahusisha wadau mbalimbali duniani ikiwemo watalam wa jotoardhi ambapo kongamano litaangazia masuala mbalimbali ikiwemo masoko ya gesi ya ukaa na upunguzaji wa gesi ya ukaa.



Ametaja Kauli mbiu ya Kongamano hilo kuwa ni, Kuharakisha Maendeleo ya Rasilimali za Jotoardhi katika Afrika, Masoko ya Gesi ya Ukaa na Upunguzaji wa Gesi ya Ukaa.

Ametaja faida za ARGeo- C10 kuwa ni pamoja na kufungua fursa zinazotokana na jotoardhi na kuharakisha maendeleo ya nishati hiyo Tazania hali itakayoongeza pia pato la Taifa na kuongeza kiasi cha umeme.



Amesema Kongamano kama hilo  lilifanyika mwaka 2014 nchini Tanzania na kuleta matokeo chanya ikiwemo uanzishwaji wa kampuni ya Jotoardhi Tanzania, Wataalam wa Kitanzania kupata mafunzo nje ya nchi na kuongeza mchango wa wadau wa maendeleo katika Jotoardhi ikiwemo Japan (JICA), Iceland, New Zealand na Marekani.

Naye, Mkuu wa Ofisi ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maziringira (UNEP) katika nchi za Kusini mwa Afrika, Meseret Teklemarian ameipongeza Tanzania kwa kuandaa Kongamano hilo kwa mafanikio makubwa.




Pia ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kulipa umuhimu mkubwa Kongamano hilo kwani maandalizi ya Kongamano husika yameshirikisha Watalam kutoka Sekta mbalimbali huku Watalam wengi kutoka Taasisi mbalimbali na mashirika binafsi wakihudhuria mafunzo yanayoendelea katka kongamano hilo.

/ Published posts: 1642

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram