Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameelekeza kurejeshwa kwa Eneo la takribani Mita za Mraba 7503 na Shilingi Milioni 500 zilizokuwa mali ya Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Arusha, Parokia ya Mtakatifu Theresia wa Mtoto wa Yesu Linalopatikana Jijini Arusha.
Kwaniaba ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda amesema hatua hiyo imefikiwa mara baada ya Mgogoro huo wa miaka zaidi ya 30 kati ya Kanisa hilo na serikali kumfikia Mhe. Rais na Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa ambapo Serikali ililichukua eneo hilo kwa matumizi yake na kisha baadae kulitaka Kanisa hilo kutoa Milioni 500 za kulipia eneo hilo wakati kanisa lilipoanza mpango wake wa kuongeza eneo la utoaji wa huduma mbalimbali kanisani hapo.
Kwa Upande wake Mhashamu Baba Askofu Dkt. Isaac Amani, Askofu wa Jimbo kuu Katoliki la Arusha, amemshukuru Rais Dkt. Samia kwa kuwa mtatuzi wa changamoto mbalimbali za wananchi huku pia akikemea Ubinafsi, Ubabe, Kutojali maendeleo ya wengine pamoja na Ulafi kwa baadhi ya watumishi wa Umma wasiokuwa waaminifu nchini Tanzania.