348 views 3 mins 0 comments

LIGI YA BASHUNGWA KARAGWE CUP 2024 YAHITIMISHWA KWA KISHINDO

In MICHEZO
August 26, 2024

Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA

Mashindano ya mpira wa Miguu ya BASHUNGWA KARAGWE CUP 2024 yaliyoanza mwezi Julai 2024 yamefikia tamati Agosti 25, 2024, kwa timu ya Nyabiyonza kuchukua ubingwa kwa mara ya tatu mfululizo baada ya kuifunga timu ya Ndama kwa goli 2-1 Katika Uwanja wa Bashungwa uliopo Kayanga Wilayani Karagwe Mkoani Kagera.

Mashindano hayo yaliyoandaliwa na Mbunge wa Jimbo la Karagwe ambaye ni Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa yalizikutanisha timu 23 kutoka kila Kata za Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe ambapo Sherehe za Fainali zilitanguliwa na mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu kati ya timu ya Nyakakika na Kihanga, ambapo timu ya Kihanga iliibuka kidedea kwa ushindi wa goli 3-0.

Akizungumza wakati akihitimisha michuano hiyo ya Bashungwa Karagwe Cup 2024, Mbunge wa jimbo la Karagwe, Innocent Bashungwa amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuhimarisha sekta ya michezo hususani mpira wa miguu.

“Na mimi niliona kwa Dira nzuri na maono ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kukuza michezo nchini, nikaona hapa Karagwe tusibaki nyuma ndio maana tunaendelea Kuboresha Ligi yetu ya Bashungwa Karagwe Cup” amesema Bashungwa.

Bashungwa ameahidi kuendelea kuboresha Mashindano yajayo ili kuwa na chachu zaidi na kuleta mafanikio kwa kuwa lengo la mashindano hayo ni kuimarisha afya kwa vijana, kusaka vipaji na kuviendeleza kwa kuunda timu ya Halmashauri itakayoshiriki katika ligi mbalimbali ndani na nje ya Wilaya ya Karagwe.

Aidha, Bashungwa amepokea ombi la kuanzishwa kwa mashindano madogo ndani ya mashindano ya Bashungwa Karagwe Cup kwa michezo ya wa Mpira wa Pete (Netball), mchezo wa Ngumi (masumbwi), na mpira wa meza (table tennis).

Naye, Mratibu wa Ligi ya Bashungwa Karagwe Cup, Johnson Majara ameeeleza kuwa mashindano ya Bashungwa Karagwe Cup 2024 ni muendelezo wa mashindano yaliyoanza tangu mwaka 2017 ambapo kwa mwaka 2024 yalishirikisha timu kutoka kata 23 za Wilaya ya Karagwe zilizopangwa katika makundi sita (6) na mpaka kufikia mchezo wa fainali ni michezo 94 iliyochezwa katika ligi hiyo.

Majara amempongeza Mbunge Bashungwa kwa juhudi kubwa za kuboresha uwanja wa Bashungwa katika viwango vizuri na kuomba uwanja huo ukamilike kwa wakati ili ligi ijayo uweze kutumika kwa michezo mingi pamoja na kusaidia kuwa chanzo cha mapato kwa Halmashauri ya Wilaya Karagwe kwa kufanyika matamasha na mashindano mbalimbali.

Mabingwa wa Bashungwa Karagwe Cup 2024, Timu ya Nyabiyonza wameibuka na Kitita cha Shilingi Milioni 6 na Medali za dhahabu, Jozi moja ya jezi pamoja na Kombe, Mshindi wa pili amejipatia Shilingi Milioni 4, Medali ya shaba na Jozi moja ya jezi huku Mshindi wa tatu timu ya Kihanga wamejipatia Shilingi Milioni 2.5, Medani ya bati pamoja na Jozi moja ya jezi.

Hali kadhalika, Mshindi wa nne timu ya Nyakakika amejipatia Tsh Milioni 1.5 ambapo Golikipa bora amejipatia Shilingi 100,000, Wafungaji bora watano kila mmoja amepatiwa Shilingi 100,000, Kwa upande wa Mchezaji bora yeye amejipatia kiatu mfano wa kombe, na kiasi cha fedha Shilingi 100,0000 wakati Mchezaji aliyecheza mchezo wa kiungwana (Fair Play) akijinyakulia zawadi ya mpira.

/ Published posts: 1614

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram