Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA ZANZIBAR
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amezishukuru Taasisi za Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA ) kwa kuonesha Wanyamapori hai kwenye Tamasha la Kizimkazi lililofanyika Kusini Unguja visiwani Zanzibar.
Ameyasema hayo leo Agosti 25,2024 kwenye Kilele cha Tamasha la Kizimkazi lililohitimishwa Makunduchi – Mweha na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali akiwemo Waziri wa Maliasili na Utalii,Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb) na Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi.
“Tunawashukuru TAWA,TANAPA, kwa kutuletea wanyama hai katika Maonesho. Ndugu zangu hawa kama walikuwa hawajui fisi basi wamemjua kwenye maonesho” amesisitiza Rais Samia.
Rais Samia alisema kuwa lengo la Tamasha hilo kubwa ni kuchochea Maendeleo ya kiuchumi na kijamii, kuwaleta watu pamoja na kudumisha Mila na desturi.
Tamasha la Kizimkazi la 2024 liliambatana na matukio mbalimbali ikiwemo uzinduzi wa miradi, kuweka mawe ya msingi ya miradi, mafunzo ya kiuchumi kwa vijana, michezo na Maonesho ya tamaduni.