225 views 53 secs 0 comments

GUTERRES AMEONYA MAUAJI YA KIONGOZI WA HAMAS YANAWEZA KUZIDISHA MACHAFUKO MASHARIKI YA KATI

In KIMATAIFA
August 01, 2024

Na Anton Kitereri

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameonya kuwa Israel kumuua kamanda wa Hezbollah mjini Beirut na mauaji ya kiongozi wa Hamas mjini Tehran yanaashiria “uzidishaji hatari” wa hali ya machafuko  huko Mashariki ya Kati.

Guterres alisema katika taarifa yake kwamba kipindi hiki “ juhudi zote zapaswa kujikita kwenye mchakato wa kusitisha mapigano katika vita vya karibu miezi 10 kati ya Israel na Hamas huko Gaza na kuongeza msaada wa kibinadamu kwa Wapalestina wanaokabiliwa na njaa, badala ya “kile tunachoona kama juhudi za kukwamisha malengo hayo.”

Guterres ametoa wito kwa pande zote kujizuia na uchochezi lakini amekiri kwamba kujizuia na uchochezi pekee yake haitoshi wakati huu mgumu sana.

“Jumuia ya Kimataifa lazima ifanye kazi pamoja kuzuia haraka vitendo vyote ambavyo vinaweza kulitumbukiza eneo lote la Mashariki ya Kati katika mzozo, ambao utakuwa na athari mbaya kwa raia,” Guterres alisisitiza.

Israel Jumanne jioni ilimuua kamanda wa Hezbollah, Fouad Shukr, katika shambulizi la anga kwenye moja ya majengo ya kundi hilo la wanamgambo katika mtaa wenye watu wengi mjini Beirut.Israel ilisema Shukr alihusika na shambulizi la mwishoni mwa juma lililoua watoto 12 na vijana waliokuwa wanacheza mpira kwenye uwanja katika milima ya Golan iliyo chini ya udhibiti wa Israel.

Saa chache baadaye, Hamas ilisema kwamba Israel ilimuua kiongozi wake Ismail Haniyeh mjini Tehran, ambako Haniyeh alikuwa amekwenda kwenye sherehe  ya kuapishwa kwa rais mpya wa Iran.

/ Published posts: 1883

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram