
Na Anton Kitereri
Takriban watu 65, wengi wao wakiwa ni watoto waliuawa tangu siku ya Jumamosi kwenye mashambulizi ya mabomu yaliyofanywa na wanamgambo wa kikosi cha Rapid Support Forces (RSF) katika mji wa jimbo la Darfur wa El-Fasher.
wanaharakati hao wamesema kwamba mji huo wa jimbo la Darfur Kaskazini ndio mji mkubwa ambao haujadhibitiwa na kundi la RSF, ambao limeuzingira tangu mwezi Mei mwaka huu.Vita kati ya RSF na jeshi la Sudan vimekuwa changamoto kubwa nchini humo tangu vilipozuka mwezi Aprili mwaka jana.
The El-Fasher Resistance Committee Jumatatu wiki walisema katika taarifa yao kwamba “ katika kipindi cha siku tatu RSF waliua zaidi ya watoto 43, wanawake 13 na wanaume tisa miongoni mwa wakazi wa El Fasher”.
“Leo ni moja ya siku za mauaji mabaya kuwahi kutokea mjini El-Fasher, dhidi ya raia, misikiti, hospitali, hasa hospitali ya Saudi”, gavana wa jimbo la Darfur Mini Minawi aliandika kwenye mtandao wake wa X.
Chanzo cha habari kutoka hospitali ya Saudi, ambayo ilishambuliwa vikali, awali kilisema shambulizi la mizinga liliua watu wapatao 22 Jumamosi.Taarifa zinaarifu kwamba RSF walipokea mfumo wa makombora kutoka El-Geneina mji mkuu wa Darfur Magharibi.
Vita nchini Sudan kati ya kikosi cha RSF kinachoongozwa na Mohamed Hamdan Dagalo na jeshi la Sudan linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, vimeua maelfu ya watu, huku makadirio yakionesha kuwa watu wapatao 150,000 wameuawa, kulingana na mjumbe wa Marekani alioko nchini Sudan bwana Tom Perriello.