145 views 2 mins 0 comments

WANANCHI WATAKIWA KITUNZA NA KULINDA MIUNDOMBINU YA BARABARA

In KITAIFA
July 19, 2024

Na Catherine Sungura,Chamwino

Ujenzi wa barabara za Chamwino  umezingatia watembea kwa miguu na wanaofanya mazoezi



Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mhandisi Victor Seff  amewaomba wananchi kutunza na kulinda miundombinu ya barabara ikiwemo taa za barabarani.

Mhandisi Seff ametoa wito huo wakati wa ukaguzi wa barabara zilizojengwa na TARURA kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya ‘Ecoroads’ wilayani Chamwino.

‘Serikali imewekeza fedha nyingi kwa kujenga miundombinu hii hivyo wananchi wanao wajibu wa kusaidia katika utunzaji na kulinda miundombinu ya barabara ili iweze kudumu kwa muda mrefu”.

Alisema wapo baadhi ya wananchi  wanaiba betri za taa  za barabarani hivyo ni wajibu wao kuzilinda na kuzitunza  taa hizo kwa manufaa ya maeneo yao.

Hata hivyo amewataka wananchi kutoa taarifa kwenye ofisi za  Wakala huo mahali popote wanapoona sehemu ya barabara ina changamoto au inahitaji matengenezo ya haraka ili wafike kutengeneza.

Aidha, Mhandisi Seff alisema kuwa ujenzi wa barabara za Chamwino umezingatia Usalama wa watumiaji wa aina zote wa barabara hususani watembea kwa miguu hivyo amewataka wananchi wanaotembea kwa miguu na wale wanaofanya mazoezi kutumia njia za pembeni za watembea  kwa miguu  ‘walkways’  ili kuepuka ajali za barabarani na  kujenga afya zao.

Naye, Bi. Rehema Mahajili mkazi wa Chamwino mtaa wa Umoja amesema wanafurahi kuona barabara zinabadilika ambapo imewasaidia kuboresha usafiri hususani kuzifikia huduma za afya na kuwaepusha kutembea kwenye vumbi kwakuwa barabara sasa hivi zimekuwa nzuri.

Barabara za Chamwino  zenye urefu wa Km. 6.95  zimejengwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya  kuboresha udongo kabla ya kuweka lami juu ijulikanayo kama ‘Ecoroads’ ambapo teknolojia hiyo  imetumika kujenga  barabara katika wilaya ya Mufindi, Rufiji  pamoja na Dodoma mjini.

/ Published posts: 1614

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram