77 views 3 mins 0 comments

TABORA JITOKEZENI KWA WINGI WAKATI WA UBORESHAJI WA DAFTARI LA MPIGA KURA

In KITAIFA
July 09, 2024

Na Mwandishi wetu WAMACHINGA TABORA
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imetoa wito kwa wananchi na wapiga kura wa mkoa wa Tabora kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kuboresha taarifa zao kwenye uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura unaotarajiwa kufanyika kwenye mikoa hiyo kuanzia Julai  20 hadi 26,2024.

Akifungua mkutano wa wadau wa uchaguzi mkoani Tabora, leo Julai 8, 2024, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Mhe.Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele amesema uboreshaji huu unamhusu kila mwananchi mwenye sifa ya kuandikishwa kuwa Mpiga Kura.

“Ni vyema mkatambua kuwa uboreshaji huu unamhusu kila mwananchi mwenye sifa ya kuandikishwa kuwa mpiga kura na anayeboresha taarifa zake. Hivyo, natoa rai kwenu kuwahimiza wananchi kupitia majukwaa yenu ya kisiasa, kijamii, kitamaduni, kiimani na kiuchumi wajitokeze kwa wingi kujiandikisha na kuboresha taarifa zao kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura,” alisema Jaji Mwambegele.

Aidha, Jaji Mwambegele alisema kuwa kila chama cha siasa kimepewa nakala ya orodha ya vituo vyote vya kuandikisha wapiga kura. Dhumuni la kuwapatia nakala hizo ni kuwawezesha kupanga na kuweka mawakala wa uandikishaji katika vituo vya kuandikisha wapiga kura.

“Kila chama kitaruhusiwa kuweka wakala mmoja kwenye kituo cha kuandikisha wapiga kura kwa lengo la kushuhudia utekelezaji wa zoezi la uboreshaji kituoni ikiwemo kuwatambua wale wanaokuja kituoni kama wana sifa za kuandikishwa,” amesema Jaji Mwambegele.

Jaji Mwambegele alitoa angalizo kwa wadau wa uchaguzi kwa umoja wao kuzingatia sheria za uchaguzi, kanuni za uboreshaji na maelekezo ya Tume kuhusu zoezi la uboreshaji wa Daftari. Huku akisema Tume kwa upande wake itazingatia Katiba, sheria ya uchaguzi na kanuni zilizotungwa chini ya sheria katika zoezi hili la uboreshaji.

Akiwasilisha mada wakati wa mkutano huo, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Kailima, R. K,  amesema mkoa wa Tabora Tume inatarajia kuandikisha wapiga kura wapya 259,989.

“Hii ikiwa ni ongezeko la asilimia 17.8 ya wapiga kura 1,463,665 waliopo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Hivyo, Tume inatarajia baada ya uandikishaji Mkoa wa Tabora utakuwa na wapiga kura 1,723,654,” alisema.

Aidha, Kailima amesema uzinduzi wa zoezi la uboreshaji wa Daftari utafanyika Mkoani Kigoma Julai 20, 2024 ambapo siku ya uzinduzi ndiyo siku ambayo pia uboreshaji utaanza katika Mikoa ya Kigoma, Tabora na Katavi na kufuatiwa na Kagera na Geita.

Ameongeza kuwa kwa lengo la kutekeleza jukumu hilo kwa ufanisi, uboreshaji kwa awamu ya kwanza utafanyika kwenye mizunguko 13 itakayobainishwa kwenye ratiba.

“Zoezi hili litaendeshwa kwa siku saba kwenye kila kituo cha kuandikisha wapiga kura. Tunatarajia zoezi litakamilika Machi, 2025,” amesema.

/ Published posts: 1215

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram