Na Mwandishi wetu WAMACHINGA
📌 *Ahimiza umuhimu wa ushirikishwaji wa Wafanyakazi*
📌 *Awataka Wakuu wa Idara na Vitengo kutoa fursa kwa Maafisa*
📌 *Asisitiza motisha kwa wanaofanya vizuri*
📌 *Dkt. Mataragio asisitiza ushirikiano na kuzingatia muda*
Katibu Mkuu wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba leo 18 Juni, 2024 amekutana na Wafanyakazi wa Wizara ya Nishati ili kujadili mafanikio ya Wizara yaliyopatikana katika kipindi cha miaka sita, kusikiliza changamoto mbalimbali za Wafanyakazi na utatuzi wake.
Katika kikao hicho kilichofanyika jijini Dodoma, Mramba amesema ni vyema Wakuu wa Idara na Vitengo wakahakikisha wanawapa fursa wafanyakazi wao ili kuwajengea uwezo kwenye utendaji wao wa kazi.
‘Kiongozi mzuri ni yule anayeruhusu wengine kukua na kuwatengeneza watu wake kwa kutoa fursa nao waweze kukua hivyo nawasisitiza msiogope kuwatengeneza maafisa wenu.” Amesema Mramba
Aidha, amewataka Wakuu wa Idara na Vitengo
kuhakikisha kuwa wanatoa motisha kwa wafanyakazi waliofanya kazi vizuri ikiwemo ya kuwatambua ili kuongeza ufanisi kwenye utendaji kazi na kuagiza kuwa utaratibu huo uanze mara moja.
Vilevile, amewataka Wafanyakazi wa Wizara ya Nishati kuheshimu kazi zao na wazifanye kwa bidii kwani ndizo zinazowabeba.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio amewataka Wafanyakazi wa Wizara ya Nishati kuhakikisha wanafanya kazi kwa ushirikiano ili kuongeza ufanisi hasa katika utekelezaji wa miradi ya nishati.
‘’ Pia niwasisitize wafanyakazi wenzangu tuwe wepesi kwenye kujifunza maana unapojifunza unaongeza ufanisi na pia tuzingatie muda kwenye utendaji kazi ili kuleta tija.” Amesema Mataragio
Akıtoa ufafanuzi juu ya masuala mbalimbali yanayohusu utawala, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Bi.Ziana Mlawa amesema jengo la Wizara ya Nishati katika Mji wa Serikali Mtumba sasa
limefikia asilimia 78.07 ambapo kwa sasa liko kwenye ukamilishwaji na hadi kufikia Septemba mwaka huu mkandarasi anatarajiwa kukabidhi jengo hilo.
Amesema kwa sasa Wizara ya Nishati ina jumla ya Wafanyakazi 211 ambapo ametumia fursa hiyo kuwakumbusha wafanyakazi kuhusu kutumia vyema mfumo wa upimaji utendaji kazi PEPMIS kwa wakati.