
Na Mwandishi wetu WAMACHINGA DAR ES SALAAM
Wakati sakata la ushoga likiendelea kutawala mijadala kupitia vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo mitandao ya kijamii, viongozi wa dini wameendelea kukemea na kutoa maonyo juu ya vitendo hivyo.
Wakizungumza na waandishi wa habari mapema leo, viongozi hao wakiwemo maaskofu, wachungaji na ma-sheikh pamoja na wakufunzi wa vyuo vya Biblia, viongozi hao wamesema suala la ushoga halihitaji kufumbiwa macho wala kusemwa kwa maneno ya kawaida.
Askofu Mkuu wa makanisa ya Ufunuo Tanzania, Paulo Bendela amesema ni muhimu kutunza na kuzingatia maadili ya vizazi vijavyo, ili waweze kuishi katika misingi yenye kumpendeza Mungu.
Askofu Bendera amesema tangu Tanzania upate uhuru, imeendelea kuwa katika misingi ya amani iliyoasisiwa na viongozi wetu, Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume.
“Nimemaikia Waziri mmoja wa kiume huko barani Ulaya akijinadi kuwa anaye mumewe, jambo ambalo halipaswi kuigwa kwani misingi na desturi zao zinaruhusu.
“Sisi viongozi wa dini tunakemea vikali, iwe ndani ya kabisa hata nje ya kanisa, tunakemea kwa nguvu za pamoja bila kujari tofauti za dini zetu,” alisema Askofu Bendera na kuongeza;
“Kwa nini tusiwe na huruma kwa vizazi vyetu? Tunaliacha Taifa la aina gani baada ya sisi kuondoka?, ni lazima tukemee tena kwa kauli moja na Serikali isaidie kusisitiza jambo hili, alisema Askofu Bendera.
Kwa upande wake Alhaji Othman Mkambaku, mwenyekiti wa Taifa wa Taasisi ya Ataqwa Charitable, inayojihusisha na ujenzi wa misikiti, uchimbaji wa visima na misaada mingine ya kijamii, amesema;
“Mwenyezi Mungu anaiadhibu Dunia yetu kulingana na machafuko na vitendo viovu tunavyovifanya sisi binadamu.
“Ninyume kabisa na mafundisho ya Mungu, lakini pia ni kinyume cha maadili, miiko, misingi, Mila na tamaduni zetu sisi Watanzania.”
Ameongeza kwa kuiomba jamii kuungana pamoja bila kujali nafasi za mtu mmoja mmoja kupinga na kukemea kwa sauti vitendo hivyo vya ushoga.