191 views 3 mins 0 comments

TANZANIA,NAMIBIA KUBADILISHANA UZOEFU KUHUSU UTATUZI WA CHANGAMOTO ZA WANYAMAPORI WAKALI NA WAHARIBIFU

In KITAIFA
May 25, 2024

Na Happiness Shayo DODOMA

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Namibia zimekubaliana kubadilishana uzoefu katika Sekta ya Maliasili na Utalii hasa katika kukabiliana na changamoto za Wanyamapori wakali na waharibifu hususan tembo wanaovamia makazi ya wananchi.

Hayo yamejiri leo Mei 24,2024 wakati wa kikao cha pamoja kati ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge la Namibia ya Maliasili waliotembelea ofisi za Wizara ya Maliasili na Utalii- Jijini Dodoma  kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu katika masuala mbalimbali yanayohusu Sekta ya Maliasili na Utalii namna inavyoendeshwa, changamoto za uhifadhi na mafanikio yake.



Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Kairuki amesema kutokana na nchi hizo mbili kuwa na changamoto zinazofanana hasa katika kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu, yuko tayari kujifunza na kuona namna ambavyo Namibia inavyotatua changamoto hizo.

Waziri Kairuki ameainisha namna ambavyo Tanzania inajitahidi kutumia mbinu mbalimbali katika kudhibiti changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu hususan tembo.



Hata hivyo amebainisha kwamba zipo sababu mbalimbali zinazochangia kuongezeka kwa migongano baina ya binadamu na wanyamapori ikiwa ni pamoja na ongezeko la watu ambao hupelekea kuongezeka kwa mahitaji ya ardhi kwa ajili ya shughuli za kibinadamu. Kutokana na kuongezeka huko kumesababisha maeneo ya shoroba za wanyamapori kuvamiwa na hivyo kuzibwa kwa mapito ya wanyamapori.

Vilvile, amesema mbinu zinazotumika kukabiliana na changamoto hizo ni pamoja na kutoa elimu kwa wananchi namna ya kudhibiti wanyamapori hao, kufukuza tembo kwa kutumia mabomu baridi ya pilipili.


Aidha, amebainisha kuwa hakuna fidia inayotolewa na Serikali bali hulipa kifuta jasho/machozi kwa waathirika ambapo hivi karibuni Wizara ya Maliasili na Utalii imefanya mapitio ya Kanuni za kifuta jasho/machozi.
Waziri Kairuki amesema Tanzania iko tayari kushirikiana na Namibia katika kufanya tafiti za namna ya kukabiliana na wanyamapori pamoja na kupeana uzoefu wa mbinu bora zaidi za kukabiliana na tembo.



Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maliasili kutoka Namibia, Mhe. Agnes Kafula (Mb) amesema Namibia iko tayari kujifunza namna bora ya kukabiliana na changamoto za wanyamapori wakali na waharibifu na kwamba wako katika mchakato wa kufanya mapitio ya Sera ili  kuanzisha bima ya maafa kwa wanaoathiriwa na  wanyamapori wakali na waharibifu.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula (Mb), Watendaji kutoka Idara ya Wanyamapori, Wizara ya Maliasili na Utalii na Afisa Bunge la Tanzania.

/ Published posts: 1614

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram