113 views 55 secs 0 comments

TUGHE NA OSHA KUSHIRIKIANA KUTOA ELIMU KWA WAFANYAKAZI

In KITAIFA
May 15, 2024

Na Mwandishi Wetu DAR ES SALAAM
———————————————
Mapema leo, Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) kimetia Saini Hati ya Mashirikiano (Memorandum of Understanding) baina yake na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) yatakayoziwezesha Taasisi
hizo mbili kushirikiana katika mambo mbalimbali hususan suala la utoaji elimu ya usalama na afya kwa wanachama wa TUGHE nchini.

Hati hiyo ya Mashirikiano imesainiwa na Katibu Mkuu wa TUGHE Taifa, Ndg. Hery Mkunda pamoja na Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda leo Jumanne tarehe 14 Mei 2024 katika Ofisi za OSHA Jijini Dar es Salaam na kushuhudiwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, *Mhe. Deogratius Ndejembi (Mb)* ambaye amezipongeza Taasisi hizo kwa kuingia makubaliano hayo yatakayokwenda kutoa elimu kwa wafanyakazi wengi kuhusiana masuala mbalimbali ya Afya na usalama katika maeneo ya kazi ili kuongeza tija.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa TUGHE, *Comrade Hery Mkunda* amesema kuwa lengo kubwa la kusaini hati hiyo ya makubaliano ni kuongeza nguvu katika kutoa elimu husuani kwa wafanyakazi kuhusu masuala yote yanayohusu usalama na Afya mahali pa kazi kwa kuzingatia sasa jambo hilo limekua haki ya msingi kwa wafanyakazi.

Naye Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda ameishukuru TUGHE kwa uamuzi huo wa kushirikiana na OSHA na kueleza kuwa utakwenda kuleta manufaa makubwa na kuleta tija katika maeneo mengi ya kazi hususani maeneo ambayo TUGHE wana matawi nchi nzima.

/ Published posts: 1214

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram