132 views 4 mins 0 comments

MKUUU WA MKOA WA LINDI AWATAKA WAKAZI WA KILWA KUWA TAYARI KUWAPOKEA WATALII

In KITAIFA
February 29, 2024



Na. Beatus Maganja

Mkuu wa Mkoa wa Lindi Mhe. Zainab Rajab Telack amewataka wakazi wa wilaya ya Kilwa na Mkoa wa Lindi kwa ujumla kuwa tayari kuwapokea watalii wanaotembelea Hifadhi ya Urithi wa Dunia ya Magofu ya Kilwa kisiwani na Songo Mnara na kutumia fursa hiyo kufanya biashara za bidhaa za utalii ili kuwaingizia kipato.

Mhe. Zainab ameyasema hayo Februari 28, 2024 akiongea na waandishi wa habari ndani ya Hifadhi ya Urithi wa Dunia ya Magofu ya Kilwa kisiwani na Songo Mnara wakati wa mapokezi ya Meli ya Saba kuingia Hifadhini humo katika kipindi cha mwezi Februari ikiwa na idadi ya watalii 120 kutoka Mataifa mbalimbali Duniani.

Amesema mfululizo wa safari za Meli za watalii ndani ya Hifadhi hiyo ni kiashiria kwamba filamu ya Tanzania The Royal Tour iliyochezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeleta matokeo chanya kwa Mkoa wa Lindi na Tanzania kwa ujumla.

Mkuu huyo wa Mkoa amesisitiza kuwa Hifadhi ya Urithi wa Dunia ya Magofu ya Kilwa kisiwani na Songo Mnara iliyo chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania – TAWA inatarajia kupokea Meli nyingine zaidi za watalii Mwezi Machi na April hivyo wakazi wa Mkoa huo watumie vyema ujio wa Meli hizo.

Aidha ametumia fursa hiyo kuwaalika watu wote wenye bidhaa zinazopendwa na watalii na kuziuza wakati wa safari za wageni ndani ya Hifadhi hiyo huku  akisisitiza kuwa TAWA imejenga jengo la kisasa na maalumu kwa ajili ya wafanyabiasha wa bidhaa za kitalii, hivyo walitumie jengo hilo ipasavyo.

Akibainisha sababu za watalii wengi kutembelea Hifadhi ya Urithi wa Dunia ya Magofu ya Kilwa kisiwani na Songo Mkuu wa Hifadhi hiyo Mercy Mbogelah amesema majengo ya kale yaliyojengwa zaidi ya miaka 1000 iliyopita kama vile msikiti mkubwa na mkongwe kuliko yote katika ukanda wa Pwani ya Afrika Mashariki na ngome ya Mreno ni vivutio vikubwa vya watalii vinavyowafanya watalii wengi kumiminika katika Hifadhi hiyo

Amesema kutokana na historia hiyo kubwa ndani ya Hifadhi ya Kilwa kisiwani  Mwaka 1981 Shirika la Kimataifa la UNESCO liliipa hadhi Hifadhi hiyo na kuwa Hifadhi ya Urithi wa utamaduni wa Dunia na baadae Mwaka 2023  kuwepa hadhi nyingine kuwa “Man and Biosphere Reserve”. Vigezo vyote hivi vimetajwa kuwa mojawapo ya sababu za watalii wengi kutoka nje kupenda kuitembelea.

Maboresho  ya miundombinu wezeshi ya utalii yaliyofanywa na Serikali kupitia TAWA nayo imetajwa kuwa miongoni mwa sababu za watalii wengi wa ndani na nje kupenda kutembelea na Kutalii ndani ya Hifadhi hiyo.

Naye Afisa Utalii wa Hifadhi hiyo, Shindawangoni Rajabu amesema Hifadhi ya Urithi wa Dunia ya Magofu ya Kilwa kisiwani na Songo Mnara imekuwa ikipokea Meli kubwa za watalii na Mwaka huu wa 2024 imepokea Meli nyingi zikiwa na idadi kubwa ya watalii katika kipindi kifupi ikilinganishwa na miaka mingine yote na inatarajia kuendelea kupokea Meli nyingine zaidi za watalii kutoka Mataifa mbalimbali Duniani.

Amesema ongezeko la idadi ya Meli zenye idadi kubwa ya watalii ni kiashiria tosha kuwa Hifadhi hiyo inaendelea kivutio kizuri zaidi Duniani.

/ Published posts: 1215

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram