277 views 2 mins 0 comments

SERIKALI ILIAGIZA NISHATI YA MAFUTA YA KUTOSHA MWAKA 2023

In KITAIFA
January 17, 2024


Na Madina Mohammed wamachinga Dodoma

Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Kapinga amesema kuwa Serikali iliagiza tani 3,036,376 za mafuta ya taa, dizeli, petroli na mafuta ya ndege katika kipindi cha mwezi Julai hadi Desemba 2023 kwa ajili ya matumizi ya ndani ya nchi pamoja na nchi jirani.

Ametoa kauli hiyo January 17, 2024 jijini Dodoma wakati wa kujadili taarifa ya utekelezaji wa Bajeti ya Wizara ya Nishati kwa Mwaka wa fedha 2023/2024 iliyowasilishwa kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.

“Katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2023 jumla ya tani 3,036,376 za bidhaa za mafuta ya dizeli, petroli, ndege na taa ziliagizwa kupitia zabuni 62 zilizotolewa na PBPA na tani 1,594,379 za mafuta hayo zilikuwa ni kwa ajili ya matumizi ya ndani na tani 1,442,000 zilikuwa kwa ajili ya nchi jirani,” amesema Naibu Waziri Kapinga.

Amesema kiwango cha mafuta kilichoagizwa kwa ajili ya matumizi ya ndani kimeongezeka kwa asilimia 4.8 ikilinganishwa na kipindi kama hicho kwa mwaka 2022 hata hivyo kiwango cha mafuta kwa transit kilipungua kwa asilimia 20.2 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2022 na sababu kubwa inatajwa kuwa ni upatikanaji wa fedha za kigeni.

Naibu Waziri Kapinga amesisitiza kuwa hadi kufikia kipindi hicho wastani wa akiba ya mafuta ya petroli nchini ilikuwa ni siku 20, dizeli siku 26 na mafuta ya ndege na taa siku 55.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Mhe. Mathayo David Mathayo ameipongeza Serikali kwa kuendelea kuwa na akiba ya mafuta ya kutosha nchini ikiwemo Petrol, dizeli, mafuta ya ndege na taa.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Mha. Felchesmi Mramba, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu Mha. Innocent Luoga na Watendaji wengine kutoka Wizara ya Nishati na Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC).

Pia, wengine walioshiriki kikao hicho ni Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Mafuta na Maji (EWURA), Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Shirika la umeme Tanzania (TANESCO), Wakala wa Nishati Vijijini (REA) pamoja na TGDC.

/ Published posts: 1614

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram