139 views 2 mins 0 comments

ULEGA AUNG’OA UONGOZI WA MNADA WA PUGU

In KITAIFA
January 03, 2024


WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amemuagiza Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. Daniel Mushi kuuondoa Uongozi mzima wa Mnada wa Pugu kwa kushindwa kufikia lengo la ukusanyaji wa mapato.

Waziri Ulega ametoa maelekezo hayo jijini Dar es Salaam alipofanya ziara katika mnada huo mapema leo Januari 3, 2024 kwa lengo la kukagua na kubaini changamoto zinazowakabili wafanyabiashara katika mnada huo.

“Naibu Katibu Mkuu ondoa uongozi mzima wa hapa mnadani, kuanzia Msimamizi Mkuu na wengine wote, leta watu wengine na hao wengine utakaowaleta uwape miezi sita kisha uniletee taarifa kama wanakidhi viwango,” alisema

“Nilileta timu hapa mwezi Disemba ikafanya kazi ya kukusanya mapato katika mnada huu, ndani ya siku 11 walikusanya zaidi ya sh. milioni 100 na hii inaonesha katika mnada huu mapato ni makubwa ila kuna baadhi ya watu wanajinufaisha,” aliongeza

Kufuatia tukio hilo, pia alimuagiza Naibu Katibu Mkuu kuhakikisha anakagua minada yote mikubwa kukagua vyema utendaji wa minada hiyo na achukue hatua pale panapostahiki ili kuboresha shughuli za sekta ya mifugo hapa nchini.

Aidha, Waziri Ulega alitumia nafasi hiyo kumuelekeza Naibu Katibu Mkuu huyo kuhakikisha ndani ya wiki moja kujenga ukuta uliodondoka katika mnada huo pamoja na kufanya ukarabati wa miundombinu ili kuboresha mazingira ya mnada huo.

Alisisitiza kuwa Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan anafanya kazi kubwa ya kuinua sekta ya Mifugo ikiwemo kufungua masoko ya biashara ya nyama nje ya nchi hivyo hatovumilia mtu yeyote anayekwenda kinyume na dhamira ya Rais.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Pugu Stesheni, Shukuru Mwinjuma alitaja changamoto ya wafanyabiashara wadogo kukamatwa na mifugo yao kwa madai sio halali wakati wanavyo vibali vyote.

Alitaja changamoto nyingine ni uhaba wa maji kutokana na mgawo kuwa mkubwa, barabara ya kuingiza mwnadani kutokuwa na kiwango cha lami jambo linalochangia wanyama wengi kuumia.

/ Published posts: 1215

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram