200 views 7 mins 0 comments

MPANGO WA USAJILI WA WATOTO WA UMRI CHINI YA MIAKA MITANO WAZINDULIWA DAR

In KITAIFA
December 09, 2023

Mpango wanufaisha watoto milioni 8.8, RITA kuendelea kusajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wa umri chini ya miaka mitano bure bila malipo

MKOA Wa Dar es Salaam umefikiwa na mpango wa usajili watoto wa umri chini ya miaka mitano ukiwa ni Mkoa wa 26 kufikiwa na mpango huo ulioanza Juni 2013 ambapo jumla ya watoto 248,298 wanatarajiwa kusajiliwa na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa bure bila malipo kupitia vituo 505 vikiwemo vituo vya afya ya ofisi za watendaji wa Kata.

Akizungumza wakati akizindua Mpango wa Usajili wa Watoto wa Umri Chini ya Miaka Mitano Mkoa wa Dar es Salaam uliofanyika katika viwanja vya Zakhiem, Mbagala jijini Dar es Salaam na kubebwa na kauli mbiu ya ‘Mtoto Anastahili Cheti cha Kuzaliwa, Mpe Haki Yake.’ Waziri wa Katiba na Sheria Balozi Dkt. Pindi Chana amesema, Rais ameiagiza Wizara ya Katiba na Sheria kupitia RITA kuhakikisha katika mikoa yote Tanzania watoto wote walio chini ya miaka mitano wasajiliwe na kupewa vyeti vya kuzaliwa bure bila malipo zoezi ambalo linahitimishwa kwa Mkoa wa Dar es Salaam.

Amesema kupitia mpango huo jumla ya watoto milioni 8.8 wamesajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa na kuhimiza wazazi na walezi kutumia fursa hiyo kwa kuhakikisha kila mtoto anapata haki hiyo katika muhimu itakayomsaidia katika shule, ajira, kusafiri pamoja na kusaidia katika kuweka mipango ya maendeleo ya Nchi.


Amesema, zoezi hilo katika jiji la Dar es Salaam limeanza vyema katika Jiji la Dar es Salaam kwa kuwa na vituo 505 zikiwemo Ofisi za watendaji wa Kata na vituo vya afya ya Mama na Mtoto na kuwataka wananchi pia kutumia siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kwa kuhakikisha kila mtoto anapata haki hiyo ya msingi bure bila malipo.

Ameeleza kuwa, katika mpango huo ulioanzishwa na Serikali kwa kushirikiana na RITA kwa kundi hilo la kimkakati Serikali inatambua jitihada za wadau wa Maendeleo wakiwemo Shirika la Kimataifa linaloshughulikia masuala ya Watoto (UNICEF,) Serikali ya Canada, Shirika la Kimataifa linaloshughulikia masuala ya wakimbizi (UNHCR,) pamoja na kampuni ya mawasiliano ya TIGO.

Pia Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Mary Makondo amesema, mpango huo ulioanza jijini Mbeya na kuhitimishwa jijini Dar es Salaam ni jitihada za Serikali ya awamu ya sita ambayo imekuwa ikitoa bajeti ya utekelezaji wa majukumu ukiwemo mpango huo unafanikiwa kwa wananchi.

Amesema, mpango huo ni mfano wa maboresho kwa kuwa huduma zimesogezwa karibu na wananchi kwa kutumia teknolojia ambayo itaongeza idadi ya watoto wengi zaidi watakaofikiwa na huduma kupitia mpango huo na hiyo ni pamoja na kuendelea kwa mpango huo mara baada ya kuhitimishwa kwake.

Kwa upande wake Kabidhi Wasii Mkuu na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili,Ufilisi na Udhamini (RITA,) Frank Kanyusi amesema, Lengo la Mpango huo ni kuongeza kasi ya ya Usajili na kutoa vyeti kwa watoto wa Umri chini ya miaka mitano pamoja na kusogeza huduma kwa wananchi kuanzia ngazi ya Kata.

“Chimbuko ya mpango huu ni kasi ndogo ya usajili, Serikali kwa kushirikiana na wadau wakaleta mpango huu ili kuongeza kasi ya usajili na utoaji wa vyeti vya kuzaliwa kwa watanzania wote.” Amesema.

Kanyusi amesema, Mpango huo una faida kwa kuwa huduma hiyo itatolewa katika vituo vyote afya vya Mama na Mtoto na Ofisi za watendaji wa Kata kwa watoto walio chini ya miaka mitano kusajiliwa na kupewa vyeti vya kuzaliwa bure bila malipo.

Amesema, mpango huo ulianza mwaka 2013 jijini Mbeya na tayari mikoa 26 imefikiwa huku wanufaika wakiwa watoto milioni 8.8 ambao wametambuliwa kupitia mpango huo na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa.

“Katika sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 katika jiji la Dar es Salaam watoto walikuwa zaidi ya laki sita, na asilimia 60.5 pekee ndio walikuwa wamesajiliwa kupitia mpango huu tumedhamiria kuwasajili watoto laki mbili arobaini na nane na mia mia mbili tisini na nane waliobaki pamoja na wale waliozaliwa baada ya Sensa.” Amesema.

Kuhusiana na mpango huo Kanyusi amesema katika jiji la Dar es Salaam awamu ya kwanza itakuwa kwa siku kumi ambapo watoto walio chini ya miaka mitano watasajiliwa na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa bure bila malipo na awamu ya pili itakuwa ya kusimika mfumo katika vituo vyote vya afya ya Mama na Mtoto ambavyo watoa huduma wamepewa mafunzo na vifaa vya kutolea huduma kwa azma yakuendeleza kutoa huduma hiyo.

Kuhusiana na changamoto ya Raia wa kigeni kuingia nchini kupitia mipakani na kujipenyeza kupata huduma hiyo Kanyusi amesema, wamekuwa wakishirikiana na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA,) Idara ya Uhamiaji, TAMISEMI na Idara za Usalama kwa kuhakikisha katika usajili lazima mzazi mmoja awe na kitambulisho cha utaifa na kueleza kuwa lengo la RITA ni kusajili kila kizazi kilichotokea Nchini bila kujali uraia.

Aidha ameishukuru wadau wa Maendeleo wakiwemo UNICEF, Serikali ya Canada, Kampuni ya Mawasiliano ya Tigo pamoja na Taasisi za Serikali kwa kuendeleza kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuhakikisha watoto wanapata vyeti vya kuzaliwa.

Wadau wa Maendeleo wakiwemo UNICEF wamepongeza jitihada za Serikali ya Tanzania ikiongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa hatua hiyo muhimu ya kusajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa ambavyo ni muhimu katika utambuzi bure bila malipo kwa watoto walio na umri chini ya miaka mitano na watanzania kwa ujumla na kuahidi kuendelea kuunga mkono jitihada hizo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadaye.

/ Published posts: 1494

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram