180 views 4 mins 0 comments

WAZIRI JAFO AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA WAWAKILISHI WA MASHIRIKA YA KIMATAIFA YANAYOFADHILI MIRADI YA MAZINGIRA TANZANIA

In KITAIFA
October 09, 2023

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amekutana na kufanya mazungumzo na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa yanayofadhili miradi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.


Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika leo Jumatatu (Oktoba 9, 2023) katika Ofisi ndogo za Ofisi Makamu wa Rais Jijini Dar es Salaam, Waziri Jafo alipokea taarifa kutoka kwa wawakilishi hao kuhusu uwasilishaji wa andiko la taarifa la vipaumbele miradi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi itakayowasilishwa katika Baraza la Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF) mwishoni mwa mwezi huu.


Waziri Jafo amesema kikao hicho na wawakilishi wa mashirika hayo sehemu ya ufuatiliaji wa maadhimio ya Mkutano Mkuu wa Saba wa Mfuko wa Mazingira wa Dunia GEF, uliofanyika katika Mji wa Vancouver nchini Canada ambapo nchi zilizoendelea na zinazoendelea zilikubaliana kuwezesha ukusanyaji wa fedha katika shughuli za uhifadhi wa mazingira duniani.


Kwa mujibu wa Waziri Jafo amesema Tanzania bado ina mahitaji makubwa ya rasilimali fedha kutoka GEF kwa ajili ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, hivyo mara baada ya kumalizika kwa kwa mkutano huo Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais iliunda timu ya wataalamu kwa ajili ya kupitia vipaumbele vya miradi ya mazingira na mabadiliko ya tabia nchi kwa ajili ya uratibu wa maombi ya fedha za utekelezaji na usimamizi wa miradi hiyo.


โ€œTanzania ni mhanga mkubwa wa mabadiliko ya tabianchi. Leo ukitazama Wilaya ya Simanjiro utaona ni kwa jinsi gani wafugaji wanavyohangaika na mifugo ya.Si hapo tu na Mpwapwa napo hali nayo si nzuriHivyo tunahitaji miradi mingi zaidi ya ufadhili wa fedha ili kuzinusuru jamii zetu”amesema Waziri Jafo.


Kwa upande wake Mshauri wa Rais, masuala ya Mabadiliko ya Tabianchi na Mazingira Dkt. Richard Muyungi ameyashukuru mashirika hayo kwa kuendelea kufadhili miradi mbalimbali ya mazingira hapa nchini na kuongeza kuwa mahitaji makubwa zaidi ya fedha bado yanahitaji ili kuleta manufaa kwa jamii na taifa kwa ujumla.


Akitolea mfano Dkt. Muyungi amesema Serikali imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali mradi ya kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwemo ujenzi wa mradi wa kingo za bahari ya Hindi katika maeneo ya barabara ya Barack Obama (Ocean Road) ambao umelenga kuzuia mmomonyoko wa udongo baharini.


Dkt. Muyungi amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali yakiwemo mashirika ya kimataifa ili juhudi za pamoja ziendelee kuimarishwa katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha miradi ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira inaendelea kuibuliwa katika jamii.


Kwa upande wao wawakilishi wa mashirika hayo wameihakikishia Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kuwa maandalizi muhimu ya uwasilishaji wa taarifa za vipaumbele vya miradi ya mazingira inayosimamiwa na GEF imekamilika na kwa pamoja wameishukuru Serikali kwa juhudi kubwa inazoendelea kufanya katika kushirikiana na wadau.


Kwa upande wake Mwakilishi wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) Bi. Clara Makenya amesema Shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuhakikisha juhudi za pamoja zinaendelea kuchukuliwa katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi ikiwemo ufadhili wa miradi na uwezeshaji wa fedha.


Miradi inayofadhiliwa na mashirika hayo ni pamoja na Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikolojia (EBARR) na Mradi wa Kurejesha Ardhi iliyoharibika na Kuongeza Usalama wa Chakula (LDFS).
MWISHO

/ Published posts: 1488

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram