Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Al-Hikma Foundation, Sheikh Nurdin Kishki amesema kati ya mabwana harusi 70 wanaofungishwa ndoa nusu yao wametoka Mkoa wa Dar es Salaam.
Hayo yamebainika wakati mkurugenzi huyo akitaja maeneo waliyopeleka mahari huku akitaja katika Jiji la Dar es Salaam wamepeleka maeneo 32 ukifuatiwa na Mkoa wa Tanga sehemu tano.
“Dar es Salaam ni Jiji la raha maeneo 32 tumepeleka mahari, nusu ya wanaharusi wanafunga leo wametoka Mkoa wa Dar es Salaam tumezunguka viunga mbalimbali kupeleka mahari,” amesema.
Amesema jumla ya mikoa 12 wakizunguka kupeleka mahari ikiwemo Dodoma maeneo ya Kondoa, Lindi, Mtwara, Pwani, Mwanza, Morogoro, Manyara, Unguja, Mara, Singida, Kigoma na Kagera.
Amesema wakati wanatangaza vijana waliojitokeza kutuma ujumbe kwa mfumo wa harafa kusaidiwa walikuwa vijana 1000 na walipofikia hatua ya kutoa fomu waliweka vigezo na masharti.
Amesema baada ya kuweka vigezo na masharti hizo jumla ya vijana zaidi 200 wajilitokeza kisha wakapewa fomu na walizirejesha na shughuli ya kuchambua nyaraka zao lilifanyika kabla ya kutangazwa uteuzi.
Amesema moja ya masharti waliyoweka ni muoaji awe bachela na shabaha ilikuwa kumsaidia asiyenacho kabisa na kigezo kingine hawe mtu aliyekosa kabisa.
“Tuliweka vigezo hivi baada ya taasisi yetu kutangazwa itagharamia suala la mahari tuliogopa watu waliooa kutumia fursa hiyo kutaka kuoa tena,” amesema.
Kigezo kingine waliweka muoaji lazima hawe na sehemu ya kujipatia riziki huku akieleza waliowengi wao kilichokuwa kina wasumbua ni kukosa fedha ya mkupuo kwa ajili ya kutoa mahari.
“Kuna ambao walikuwa wanataka kuozesha watoto wao kuanzia Sh800,000, Sh1milioni na wengine hadi Sh2.5 milioni na baadhi walikuwa wanahitaji kabati na vitu vingine,” amesema.