Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Masuala ya Usawa wa Jinsia, Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Familia kutoka Bunge la Namibia wameipongeza Serikali kwa kuimarisha huduma za matibabu ya moyo jambo ambalo limewafanya watanzania na mataifa mengine kutibiwa moyo hapa nchini.
Pongezi hizo zimetolewa na wabunge hao jijini Dar es Salaam wakati walipotembelea Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwaajili ya kuona huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa pamoja na kujifunza jinsi ambavyo Tanzania imefanikiwa katika kutoa huduma za matibabu hayo.
Kiongozi wa msafara wa wabunge hao Julieta Kavetuna alisema kufika kwao katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wamejifunza mambo mengi ikiwa ni pamoja na kuona mitambo na vifaa tiba vya kisasa vya kutoa huduma za matibabu ya moyo.
“Nchini Namibia hatuna Taasisi ya Moyo kama hii sisi tuna idara ya magonjwa ya moyo ambayo iko katika Hospitali ya Taifa, lakini kama Serikali ikiamua tunaweza kuwa na Hospitali ya moyo inajitegemea ambayo itakuwa inatoa huduma za matibabu ya kibingwa kwa wagonjwa”.
“Vitu tulivyojifunza hapa ikiwa ni pamoja na kusomesha wataalamu, kufanya kazi kwa pamoja, kutoa huduma bora kwa wagonjwa na kununua vifaa tiba vya kisasa tutakwenda kuvifanyia kazi Namibia, ninaamini miaka michache ijayo nasi tutakuwa na Hospitali ya moyo”, alisema Julieta.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Upasuaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt.Anjela Muhozya alisema tangu kuanzishwa kwa Taasisi hiyo mwaka 2015 idadi ya wagonjwa wa ndani na nje ya nchi imekuwa ikiongezeka hii ni kutokana na kuwa na wataalamu wa kutosha pamoja na vifaa tiba vya kisasa.
Dkt. Angela alisema ili kuongeza ujuzi wataalamu wa Taasisi hiyo wamekuwa wakifanya kambi maalumu za matibabu na upasuaji wa moyo kwa kushirikiana washirika wao kutoka mataifa mbalimbali yaliyoko katika Bara la Ulaya, Marekani, Australia na Asia.
“Tunaishukuru Serikali ambayo imekuwa ikituunga mkono kwa mambo yote tunayoyafanya kwani imesomesha wataalamu,kutujengea majengo na kutununulia vifaa tiba nasi kama wataalamu tunahakikisha watu wenye matatizo ya moyo wanapata huduma bora na kwa wakati”.
“Taasisi yetu inatoa huduma ya tiba mkoba ya kuwafuata wananchi mahali walipo tunatoa huduma hii kwa kushirikiana na wenzetu wa hospitali husika. Wakati tunatoa huduma hii tunafanya mafunzo ya kuwajengea uwezo wataalamu wa afya ili waweze kuwatambua na kuwatibu wagonjwa wa moyo kwa kufanya hivi wagonjwa wanatambuliwa mapema na kupata huduma kwa wakati”.alisema angela
Hata hivyo Taasisi hiyo pia imekuwa ikipokea wagonjwa kutoka nchi zinazopakana nazo mipaka zikiwemo za Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Somalia, Sudani, Zambia, Congo, Malawi, Msumbiji, Zimbabwe na Visiwa vya Comoro