172 views 3 mins 0 comments

RC SENYAMULE ATOA WITO KWA VIJANA MKOA WA DODOMA KUCHANGAMKIA FURSA YA AFYA BONANZA KUPIMA AFYA ZAO.

In KITAIFA
June 15, 2023

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule ametoa wito kwa vijana kuchangamkia fursa za Afya Bonanza ili waweze kupima afya zao na kupata elimu kuhusu masuala mbalimbali ya afya.

Akitoa wito huo Mkuu wa mkoa Rosemary Senyamule katika ufunguzi wa Bonanza la Afya Mkoa wa Dodoma uliofanyika katika shule ya Msingi Chang’ombe na kufanikiwa jumla ya watu 721 hasa vijana kufikiwa na elimu kuhusu masuala mbalimbali ya afya.

“Nikipiga hesabu za haraka haraka ,tunategemea katika bonanza hili kufikia vijana 6000 katika mkoa wa Dodoma kwa kata 28,tumieni fursa kuja kushiriki bonanza hili ili kupata elimu ya afya kwa vijana na huduma zinazotolewa kwa Jiji la Dodoma ,na kila mmoja akielimisha kijana tutafikia vijana 30,000”amesema Senyamule.

Aidha,Mkuu wa Mkoa Senyamule amesema mada zinazotolewa ikiwemo elimu ya afya ya uzazi,lishe, ukatili wa Kijinsia ina umuhimu mkubwa katika makundi mbalimbali ya watu hususan Vijana.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Watoto na Vijana kutoka Wizara ya Afya Dkt.Felix Bundala amesema kama Wizara wameamua kuwekeza nguvu zaidi kufikisha elimu ya afya na huduma kwa vijana ikiwemo namna ya kujikinga na UKIMWI na Mimba za Utotoni.

“Tumeamua kuangalia namna ya kufikisha elimu kwa vijana ikiwemo mimba za utotoni,ukatili wa kijinsia,Magonjwa yasiyo ya Kuambukiza ,lishe ,Madhara ya dawa za kulevya,afya ya akili”amesema bundala

Nae Mganga Mkuu Mkoa wa Dodoma Dkt.Best.Magoma amesema kutakuwa na matokeo chanya katika bonanza hilo.

Nao baadhi ya vijana wa Chang’ombe akiwemo Furaha David, Juma Athuman, pamoja na Mwajuma Hassan wamesema bonanza hilo limekuwa na manufaa makubwa kwao huku wakiiomba Wizara ya Afya kuendelea kuwezesha mabonanza kama hayo mara kwa mara .

“Kwa kweli kupitia bonanza hili la Afya nimeipongeza Wizara ya Afya kwanza imenipunguzia gharama Kwenda hospitalini lakini hapa vipimo nimepata bure na elimu ya afya imekuwa na msaada kwangu kujua namna cha kufanya”amesema Furaha David.

Ikumbukwe kuwa katika bonanza hilo la Afya mbali na utoaji wa elimu na huduma, michezo mbalimbali imefanyika kwa vijana ikiwemo mpira wa miguu,pete,kukimbiza kuku huku jumla ya watu 721 kata ya Chang’ombe wakifikiwa elimu ya afya kupitia bonanza hilo .

Halikadhalika, katika bonanza hilo la afya kupitia Wizara ya Afya ,Idara ya Huduma za Mzazi, Mama na Mtoto kwa kushirikiana na Elimu ya Afya kwa Umma,Ofisi ya Rais-TAMISEMI, chini ya uwezeshaji wa Mfuko wa Dunia( Global Fund) linafanyika katika mikoa mitano(5)halmashauri 18 lengo ni kufikia watu 15,000 katika mikoa hiyo,watu 833 kila Halmashauri na watu 208 katika kila kata .

Kwa mkoa wa Dodoma malengo ni kufikia watu 500 kila kata ambapo Kata ya Chang’ombe imevuka lengo na kufikia watu 721 na siku ya Juni 15.2023 bonanza litaendelea katika kata ya Kikuyu.

/ Published posts: 1480

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram