Tanzania na Kenya ziko katika kikao cha majadiliano ya kuendelea na kazi kuimarisha mpaka wa kimataifa wa nchi hizo mbili kipande cha awamu ya tatu cha kutoka Namanga mkoani Arusha hadi Tarakea Kilimanjaro.
Kikao hicho cha siku tano cha Kamati ya Pamoja baina ya Wataalamu wa nchi hizo mbili kilianza tarehe 29 Mei 2023 na kutarajiwa kukamilika ijumaa tarehe 2 Juni 2023 kikiwa na lengo la kupokea taarifa ya ukaguzi wa kipande cha awamu ya tatu cha km 110 kutoka Namanga mkoani Arusha hadi Tarakea, Kilimanjaro, kufanya ukaguzi wa eneo linaloimarishwa na kuandaa mpango kazi wa awamu zinazofuata.
Akifungua rasmi kikao cha Kamati hiyo ya Pamoja tarehe 31 Mei 2023 jijini Arusha kwa niaba ya Mkuu wa mkoa huo John Mongela, Kaimu Katibu Tawala wa mkoa huo David Lyamongi alisema, kikao hicho kinadhihirisha umuhimu wa kazi walioyopewa wataalamu wa nchi hizo mbili kwa kuhakikisha kazi waliyopewa inakamilika katika muda uliopangwa.
โโNinafahamu timu ya wataalamu wa pande zote mbili zimekuwa na vikao ambapo kikao cha mwisho kilifanyika mwezi Desemba 2022 mjini Kajiado nchini Kenya na kufuatiwa na ukaguzi awamu ya tatu ya kipande cha kuanzia Namanga hadi Tarakea pamoja Tarakea hadi ziwa Jipeโโ alisema Lyamongi
Wakiwa katika eneo hilo, timu hiyo ya wataalamu ya Kamati ya Pamoja ya nchi hizo wakioongozwa na Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani Hamdouny Mansoor kwa upande wa Tanzania na Mtendaji Mkuu wa Ofisi ya Mipaka ya Kimataifa ya Kenya (KIBO) Juster Nkoroi walijionea uhalisia wa mpaka pamoja na changamoto za eneo hilo wakati wa ukaguzi.