Meneja wa Bandari ya Tanga, Masoud Athumani Mrisha akizungumza na Waandishi wa Habari
Baada ya maboresho makubwa hatimaye bandari ya Tanga imeanza kupokea meli kubwa, huku shehena za mizigo pia zikiongezeka kutoka tani laki saba na nusu mpaka tani milioni 3 kwa mwaka, pia ikioneka kuanza kuichangamsha mikoa mingi ya jirani hasa ya Kaskazini.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Mei 25, 2023, Meneja wa bandari hiyo, Masoud Athumani Mrisha amesema baada ya maboresho hayo mpaka sasa wameshaingiza meli sita zenye urefu mita kati ya 150 mpaka 200 kwa kipindi cha miezi mitatu, ambazo hapo awali hazikuweza kutia nanga bandarini hapo kutokana na kina kidogo cha maji, huku akiwataka wateja wa mikoa hiyo ya Kaskazini na nchi jirani waitumie kwakua imezaliwa upya baada ya maboresho.
“Kabla ya maboresho ya bandari yetu kwa mwaka tulikuwa tunapokea shehena tani laki saba na nusu, lakini baada ya maboresho haya sasa tunakwenda mpaka tani milioni 3 kwa mwaka, pia gharama za uendeshaji zimepungua kwa maana ya kupakia na kushusha mizigo kutoka meli kubwa kwenda Matishari kisha kushusha tena. Vilevile zamani tulihudumia meli moja kwa siku nane sasa tunaihudumia kwa siku nne. Hata kodi sasa itapatikana kwa wingi kwakuwa shehena imeongezeka,” alisema Mrisha.
Akiongelea mchakato mzima wa upanuzi wa bandari hiyo ulivyokuwa Meneja Mrisha amesema, Serikali kupitia Mamlaka ya Bandari nchini ilianza mradi wa kuboresha bandari ya Tanga kwa awamu mbili. Awamu ya kwanza ilianza tarehe 3/8/2019, awamu hiyo ilikuwa ni ya kipindi cha mwaka mmoja, ilikua ni kuongeza kina cha maji kwenye mlango bahari, kutoka mita 3 mpaka 13, huku upana wa mlango ukienda mpaka mita 73.
“Vile vile kuongeza kina cha maji sehemu ya kugeuzia meli (turning base) kutoka mita 3 mpaka 13 kwa kipenyo cha mita 800, pia awamu ya kwanza ilijumuisha ununuzi wa vifaa hivi mnavyoviona, ziwemo mashine za kubeba kontena zenye uwezo wa kubeba tani mia kila moja, forklift ya tani 50 kubwa na mbili za tani 5, mashine ya kubebea kotena tupu na vingine.
“Mradi wote huo wa awamu ya kwanza uligharimu bilioni 172.3 na kukamilika kwa asilimia100, ambapo mradi wa pili ulikua ni kuboresha gati mbili iliyojengwa mwaka 1914 na ile ya mwaka 1954 zenye urefu wa mita 450, kilichofanyika upande wa Mashariki tuliingia majini mita 50, Magharibi tukaingia mita 92 kwenye maji na tukaongeza kina cha maji kutoka mita 3 mpaka 13, mradi huo awamu ya pili ulianza tarehe 5/9/2020, ulikuwa ni wa miezi 22 na thamani yake ni bilioni 256.8, mpaka sasa umekamilika kwa asilimia 99.85, hizo asilimia 0.15 ni vitu vidogo ambavyo tunasubiria kukamikika,” alisema.
Kuhusu historia ya Bandari ya Tanga kwa ufupi Meneja Mrisha alisema, ilianza kujengwa mwaka 1888 na kukamilika 1891, kipindi hicho ilijulikana kama Marine Jet. Gati la kwanza lilianza kujengwa 1914 na gati la pili lilijengwa 1954, yote hayo yalikua na urefu wa mita 450.
“Bandari ya Tanga inaukubwa wa hekta 17, lakini pia tuna maeneo mengine, eneo la Mwambani kilomita sita kutoka hapa ambalo lina hekta 176 na Chongoleani linakojengwa bomba la mafuta kilomita 28 kutoka hapa lenye ukubwa wa hekta 207.
“Bidhaa kubwa tunazosafirisha kupitia bandari yetu ya Tanga ni pamoja na Katani, Kahawa, mbao na Makademia (Karanga pori) na tunazopokea kutoka nje ya nchi kupitia bandari yetu ni pamoja na mafuta, vipuri mbalimbali vya magari (spare parts), malighafi za viwandani n.k.
“Muda wote huo tokea mwaka 1891 ilipokamilika bandari yetu ya Tanga tulikua tunafanya kazi angani, yaani meli kubwa inakuja kilometa 1.7 inasimama nje ya bandari, inapakua mzigo na kuhamishia kwenye Matishari ambayo hukokota na kuuleta hapa gatini kwasababu ya kina kifupi cha maji kilichokua hapa gatini,” alisema Mrisha.