8 views 3 mins 0 comments

YST YAPOKEA MAOMBI 1516 YA WANASAYANSI CHIPUKIZI

In KITAIFA
April 29, 2025



Na Penina Malundo

SHIRIKISHO la Wanasayansi Chipukizi (YST),limepokea idadi kubwa ya maombi ya kazi za kisayansi kutoka kwa wanafunzi  kushiriki mashindano ya sayansi yanayofikia 1,516 kwa mwaka 2025 ukilinganisha na mwaka uliopita mapmbi 1055.

Aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, Mwanzilishi Mwenza wa YST Dk. Gozibert Kamugisha  wakati akiongea na waandishi wa habari  juu ya mashindano hayo yanayotarajiwa kufanyika Septemba 18, 2025 katika eneo la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Amesema  idadi hiyo ya wanafunzi imefanya kuwepo kwa ongezeko la asilimia 43 kwa kazi za kisayansi zilizowasilishwa mwaka huu.

“Ongezeko hili ni matokeo ya mpango imara wa mafunzo ya kisayansi shuleni unaoendeshwa na YST katika mikoa yote ya Tanzania ambao kwa mwaka huu umeshirikisha wanafunzi 6,064 na walimu wa sayansi 402.

“Ambapo mpango huo wa mafunzo ya kisayansi shuleni bado unaendelea na hatimaye zitachaguliwa kazi za sayansi  zipatazo 360 zitakazoendelea kupatiwa mafunzo katika duru ya pili ili kuhakikisha kazi za sayansi zitakazoonyesha katika mashindano ya YST 2025 ni za ubora wa kiwango kinachoridhisha,” alisema Dkt Kamugusha

Aidha amesema mpango wa mafunzo ya sayansi shuleni mwaka huu utahitimishwa kwa kuchagua kazi za kisayansi 55 zenye ubora wa kiwango cha juu ambazo zitaonyeshwa kwenye maonesho ya YST 2025 yatakayofanyika UDSM Septemba 18, mwaka huu,” amesema

Hata hivyo Dk. Kamugisha amesitiza kuwa dhumuni la kufanya maonesho hayo UDSM ni kutengeneza jukwaa la kuwaleta pamoja wanasayansi chipukizi kutoka shule za sekondari la kuwakutanisha na wanasayansi wabobevu kutoka chuo hicho kikuu na vingine ili kupata ushauri juu ya namna bora ya kuboresha gunduzi zao.

“Mpango huu wa kuibua na kulea vipaji vya kisayansi kwa vijana unadhaminiwa na Karimjee Foundation (KFI) / Toyota Tanzania. Tunaamini kupitia mpango wetu huu vijana ambao ni wanasayansi chipukizi wataendelea kuhamasika zaidi katika kufanya gunduzi mbalimbali za kisayansi.” Amesisisitiza.

Kwa upande wake Ofisa Mkuu wa Masoko Karimjee Foundation, Cobus van Zyl amesema tangu mwaka 2012  ,Taasisi yao imekuwa mdhamini mkuu wa mashindano hayo ambapo kila mwaka wamekuwa wakitoa ufadhili wa masomo ya elimu ya juu kwa wanafunzi ambao wameshinda katika kundi la washindi wa jumla na kundi maalum la elimu.

“Mafanikio haya ni fahari kubwa kwetu kuanzia katika taaluma za uhandisi na sayansi ya Afya hadi uhifadhi wa mazingira na sera.

Ushirikiano huu ni mfano wa jitihada wa uwajibikaji wa  Taasisi yetu ya Karimjee Foundation na YST ambao kwa pamoja unaonesha dhamira ya kukuza elimu nchini hususani sayansi na teknolojia kwa vijana.

“Kwa kushirikiana na timu ya YST hatuwekezi tu kwa wanafunzi bali tunajenga utamaduni wa kitaifa wa kutafiti, kujenga, ubunifu na kuleta suluhu ya matatizo yaliyopo kwenye jamii,” amesisitiza  Zyl

Amesema hadi sasa wahitimu 49 wa YST ambao ni vijana  wamepokea ufadhili wa masomo kutoka Karimjee Foundation kwa lengo la kuboresha maisha yao.

Naye Mshindi wa Jumla wa mashindano hayo mwaka 2018 kutoka Shule Sekondari Wasichana Msalato, Farida Mnyazi amesema kutokana na kushinda alifanikiwa kupata ufadhili kutoka Karimjee Foundation ambao umemsaidia kupata elimu ya juu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

/ Published posts: 1975

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram