
Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA
Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO) imekamilisha ujenzi wa Mradi wa laini ya msongo wa Kilovolti 132 yenye urefu wa kilomita 102 kutoka Tabora hadi Ipole, ambao utawasaidi Wananchi wa Wilaya ya Sikonge kupata huduma ya Umeme wa uhakika na kuchochea maendeleo.
Akizungumza leo, Aprili 27, 2025, Mkoani Tabora katika zoezi la kuwasha laini hiyo mpya, Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya ETDCO, CPA. Sadock Mugendi, amesema kuwa ujenzi wa laini hiyo umekamilika kwa asilimia 100, hivyo Wananchi wa Ipole, ambapo kwasasa Wananchi wa Wilaya ya Sikonge wanapata Umeme wa uhakika baada ya kukamilisha zoezi hilo majira ya saa tisa Alasiri.
CPA. Mugendi ameishukuru Serikali na Wizara ya Nishati kupitia TANESCO kwa kuwaamini kutekeleza Mradi huu, huku akieleza kuwa wapo hatua za mwisho za kukamilisha kipande cha pili cha Mradi kutoka Ipole hadi Wilaya ya Mlele, Mkoani Katavi wenye urefu wa takribani kilomita 133.
CPA. Mugendi ametoa wito kwa Wananchi kuhakikisha wanatunza Miundombinu ya Mradi huo kwani Serikali imetumia gharama kubwa kutekeleza Miradi kwa manufaa ya Wananchi na Taifa kwa ujumla.
Meneja wa Mradi kwa upande wa TANESCO, Mhandisi Sospeter Oralo, amesema kuwa Mradi wa Tabora hadi Katavi umegharimu jumla ya shilingi bilioni 161, ambapo awamu ya kwanza umekamilika na Wananchi wa Wilaya ya Sikonge wataweza kupata Megawatts 12 kupitia njia mpya ya msongo wa Kilovolti 132.
Amewasihi wananchi wa Wilaya ya Sikonge kutumia Umeme huu kama fursa kwa kufanya uwekezaji katika shughuli mbalimbali za kiuchumi ili kuboresha vipato vyao, huku akisisitiza matumizi ya Nishati safi ya Umeme majumbani, ambayo inasaidia kupunguza gharama na kuboresha afya pamoja na Mazingira.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Mradi wa Tabora hadi Katavi upande wa ETDCO, Mhandisi Ebenezer Makakala, amesema kuwa Wananchi wa maeneo ya Mradi wamefaidika kwa kupata fursa ya kufanya kazi kama vibarua wakati wa utekelezaji wa Mradi.
Nao, Vibarua wa mradi huo, akiwemo Mateo Daudi, wameeleza shukrani zao kwa Serikali kwa kuleta Mradi huo, kwani umekuwa na manufaa makubwa kwao, ikiwa ni pamoja na kuwasaidia kuingiza kipato kilichowasaidia kugharamia mahitaji ya familia zao, ikiwemo kulipa ada kwa watoto wao.