




Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA
Watumishi wa umma ni taswira au sura ya Serikali hivyo tunatakiwa tuangalie na kuzingatia namna tunavyofanya kazi na tunapotekeleza majukumu ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa niaba ya Serikali. Kila mmoja ana wajibu kwa kutunza taswira ya Serikali tunayoitumikia chini ya Uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hayo yamesemwa na Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Bi. Alice Mtulo wakati anafunga mafunzo elekezi kwa watumishi wapya wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali yaliyofanyika Kibaha mkoani Pwani kwa muda wa siku tano.
Bi. Mtulo amewaeleza watumishi hao kuwa Serikali ina sheria, taratibu na kanuni zinawapa mwongozo wa namna ya kufanya kazi kama mtumishi wa umma ambapo katika hayo maadili ya utumishi wa umma, yanatuasa kuhusiana na rushwa.
“Sisi ni Mawakili wa Serikali, tunaendesha mashauri yenye maslahi mapana ya Serikali ambapo mashauri hayo yana kiwango kikubwa cha fedha na yanahusisha watu mbalimbali ndani na nje ya nchi, hivyo Mawakili wa Serikali tujiepushe na rushwa. Aidha, inapotokea unakutana na mazingira ya rushwa, kimbia ili kulinda taswira ya taasisi na Serikali; heshima, utu na haiba yako kwa jamii na watu wanaokutegemea,” amesisitiza Bi. Mtulo.
Bi. Alice Mtulo amewataka Mawakili hao kutunza siri za Serikali kwa kuwa majukumu wanayotekeleza yanawapa nafasi ya kufahamu taarifa mbali mbali. “Jinsi unavyotunza siri zako, una wajibu wa kutunza siri za Serikali, tuwe waangalifu katika hili.Ukikutwa umevujisha taarifa za Serikali utachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria,” amefafanua Bi. Mtulo.
Aidha, amewaasa Mawakili hao kuzingatia mawasiliano na uhusiano baina yao na viongozi, watumishi wengine na wadau wanaofanya nao kazi. Alisisitiza kuwa na mipaka kwa kuzingatia taratibu za Ofisi ikiwemo kuwa makini kwa yale wanayoandika na kuongea ikiwa ni pamoja na kufuata sheria, kutumia hekima na busara, kuwa waaminifu na wasikivu kwa Serikali tunayoitumikia.
“Sipo tayari kumvumilia mtu yeyote asiyekuwa na nidhamu kwake yeye mwenyewe, wenzake na kwa kiongozi wake.
Vile vile, ametoa rai kwa Mawakili hao kuzingatia na kutumia mifumo ya TEHAMA kwa kuwa Serikali imejikita kwenye matumizi ya mifumo ya TEHAMA. Ofisi ina mifumo mbalimbali ya TEHAMA ambapo kila mtumishi atapimwa utendaji kazi wake kupitia mifumo hiyo. Alisisitiza kila mmoja anapaswa kujaza taarifa za utekelezaji wa majukumu kupitia mifumo hiyo. “Ukitoka Mahakamani jaza taarifa kwenye mifumo husika ili Ofisi ipate takwimu sahihi na kwa wakati.” Aidha alisisitiza kuhusiana na dhumuni na wajibu wa kila mmoja kwa Ofisi, wajibu kwa wafanyakazi wenzako na wajibu kwako wewe binafsi. “Kumbuka na tafakari kuwa ulikuja Ofisini peke yako, usifuate mikumbo na usiwe mwanaharakati. Zingatia sheria, taratibu na kanuni za utumishi wa umma, endapo una mahitaji ya msingi wasilisha kwa mamlaka husika kwa utaratibu uliowekwa na yatafanyiwa kazi,” amefafanua Bi. Mtulo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Ofisi hiyo, Bi. Asha Hayeshi amewaeleza Mawakili hao kuwa ni muhimu kwa Wakili wa Serikali kutekeleza majukumu yake kwa kushirikiana na watumishi wenzake ili kurahisisha mgawanyo wa majukumu na matumizi bora ya ujuzi kwa kila mmoja wakati wa kuandaa majibu ya mashauri ya Serikali, kuchambua ushahidi kwa kina na kuhakikisha mashauri yanaendeshwa kwa ufanisi mkubwa kwa maslahi mapana ya Serikali.