10 views 2 mins 0 comments

SAMIA KALAMU AWARD KUTOLEWA APRIL 29

In KITAIFA
April 15, 2025


Na Aziza Masoud, Dar es Salaam


CHAMA Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kimesema hafla ya utoaji tuzo za uandishi wa habari za maendeleo, maarufu kama Samia Kalamu Awards itafanyika April 29 mkoani Dodoma.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkurugenzi Mkuu wa TAMWA Dk. Rose Reuben alisema hafla ya utoaji tuzo hizo inatarajiwa kufanyika Aprili 29, 2025, katika Ukumbi wa Mabele, Mabeyo Complex jijini Dodoma, ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan.

“Tuzo hizi zimebuniwa kwa lengo la kuhamasisha uandishi wa habari unaojikita katika maendeleo kwa kufanya uchambuzi wa kina, kuimarisha maudhui ya ndani, na kuzingatia maadili, weledi na uzalendo kwa ajili ya kujenga taswira chanya ya Taifa.

” Tukio hilo litarushwa mubashara kupitia vituo mbalimbali vya televisheni, redio na mitandao ya kijamii ili kuruhusu wananchi kushuhudia washindi wakituzwa mbele ya Mgeni Rasmi, ikiwa ni ishara ya kuthamini mchango wa wanahabari nchini, ” alisema Dk.Rose.

Alisema tuzo hizo ni matokeo ya mafunzo yaliyofanyika mwaka 2024, yakilenga kukuza uandishi wa habari za maendeleo. Washiriki walituma kazi zao zilizorushwa au kuchapishwa kupitia vyombo mbalimbali vya habari.

Alisema tuzo zimetengwa hizo katika makundi matatu ambazo ni Tuzo Maalumu za Kitaifa ikiwemo Tuzo ya Chombo cha Habari Mahiri Kitaifa, Mwandishi Bora, Afisa Habari Mahiri wa Serikali, na Tuzo za Nishati Safi ya Kupikia.

Alisema tuzo nyingine ni tuzo kwa vyombo vya habari ambao zitatolewa kwa vyombo vya Televisheni, Redio (Kitaifa na za Kijamii), Magazeti na Vyombo vya Habari Mtandaoni.

Alisema pia kuna tuzo za kisekta kwa waandishi waliobobea kwenye sekta za afya, elimu, maji, kilimo, mazingira, jinsia, utalii, madini, uchumi wa buluu, TEHAMA, michezo, sanaa na nyinginezo.

TAMWA na TCRA zimewahimiza waandishi na vyombo vyote vya habari kushiriki kikamilifu katika hafla hiyo ya kihistoria kwa ajili ya kusherehekea na kutambua kazi ya wanahabari katika maendeleo ya taifa.

/ Published posts: 1913

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram