
Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA
*• Kuchangia Namungo ni hiari msirudi nyuma ichangieni*
*•Apongeza jitihada za Rais kukuza michezo na timu kuwa na uwanja kisasa*
LINDI: KATIBU wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi, Uenezi na mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), CPA Amos Makalla amesema wasichoke kuichangia timu ya Namungo inapohitajika, kwani uwepo wa timu hiyo unaleta utalii wa michezo unaosaidia kukuza uchumi katika Wilaya ya Ruangwa na Mkoa wa Lindi kwa ujumla
Makalla ameeleza hayo leo Aprili 13, wakati akizungumza katika mkutano wa ndani na wananchi wa Wilaya ya Rwangwa mkoani Lindi ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya siku 10 katika mikoa ya Lindi na Mtwara.
Makalla amesema kuwa uwepo wa uwanja Ruangwa ni fursa kwa wananchi wa wilaya hiyo hususani katika msibu waligi kuu kwa sababu timu 15 zinafika katika uwanja huo kwa ajili ya michuano ya ligi kuu na kusaidia wafanyabiashara wadogo na wakubwa kujiendeleza kiuchumi kwa kutoa huduma wageni.
“Uwepo wa Timu ya Namungo kiuchumi tunasema kuna utalii wa kimichezo yaani timu zote 15 lazima zikajaze uwanja na katika kujaza uwanja hoteli zinajaa, bodaboda wanabeba mashabiki, wasioweza kula hotelini watakula kwa mama ntilie biashara zetu zinaongezeka,” amesema Makalla.
Pia Makalla amesema kuwa suala la michango ni hiyari na kama wananchi wanaipenda timu ya Namungo basi wasichoke kuichangia kutokana na umuhimu wa kuwepo kwa timu hiyo kwa wananchi wa Rwangwa.
“Mimi nilikuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza nimekuta pamba ina miaka 22 haijwahi kupanda ligi kuu kwa sababu napenda na nimecheza mpira nimekaa Mwanza miezi nane tu nikapandisha timu ya Pamba, sikupandisha kwa hela zangu wala za serikali ni wananchi wa mkoa wa Mwanza,” amesema Makalla.