18 views 2 mins 0 comments

KAIMU  KATIBU MKUU DAUDI AWAFUNDA WAJUMBE WA KAMATI ZA USHAURI ZA AJIRA ZA RAIA WA KIGENI KATIKA UTUMISHI WA UMMA

In KITAIFA
April 09, 2025



Na. Lusungu Helela – Dodoma.

Kaimu  Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi amewataka Wajumbe wa Kamati za Ushauri za Ajira za Raia wa Kigeni katika Utumishi wa Umma kuhakikisha wanalinda taswira ya nchi kimataifa kwa kuyafanyia kazi na kuyawasilisha maombi hayo ya ajira za raia wa kigeni kwa wakati katika Ofisi ya Rais, UTUMISHI na Utawala Bora.

Amesema Kamati hizo kwa uzembe wake zimekuwa zikiharibu mahusiano ya kidiplomasia ya kimataifa kwa kufanya kazi kwa mazoea katika kushughulikia suala hilo nyeti la ajira za raia wa kigeni kwa kuwasilisha maombi hayo  yakiwa yamechelewa na hayana viambatisho muhimu, hali inayochangia kuipa wakati mgumu Ofisi ya Rais, UTUMISHI katika kuyafanyia kazi.

Bw. Daudi ametoa kauli hiyo leo wakati akifungua mafunzo elekezi kwa Wajumbe wa Kamati hizo kwa  ngazi ya Wizara yanayofanyika kwa muda wa siku mbili   katika Ukumbi  wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.

“Tumekuwa tukipokea kila aina ya lawama kuwa sisi Ofisi ya Rais, UTUMISHI na Utawala Bora ndio tunakwamisha mchakato ambapo wakati mwingine unakuta hata maombi hayo bado hayajawasilisha kwetu, hili jambo sio zuri badilikeni” amesisitiza Kaimu Katibu Mkuu Daudi.

Amesema Wajumbe wa Kamati hizo ambao hawatimizi jukumu hilo nyeti walilopewa wanapaswa kujisikia  vibaya huku akiwataka kuacha tabia hiyo ya kufanya kazi kwa mazoea.

Amefafanua kuwa maombi hayo ya ajira yamekuwa hayawasilishwi kwa wakati na wakati mwingine yamekuwa yakiwaletwa Ofisi ya Rais, Utumishi ikiwa tayari raia hao wa kigeni wakiwa wameshawasili nchini, jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa nchi na ni kinyume cha sheria.

Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu, Bi. Sophia Abdallah amesema wamelazimika kufanya mafunzo hayo  kwa lengo la kuwakumbusha wajumbe hao  juu ya wajibu wao wa kuyafanyia kazi na kuyawasilisha  kwa wakati maombi hayo yakiwa na nyaraka zote zinazotakiwa ili kuondoa mkwamo huo. 

Ameongoza kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa wajumbe hao ikizingatiwa kuwa kwa sasa Tanzania haina uhaba wa wataalamu kama ilivyokuwa hapo awali, hivyo mafunzo hayo yanatumika kuwakumbusha kuwa makini katika uchambuzi wa maombi watakayokuwa wakiyawasilisha kwa kuangalia uhaba halisi wa ajira hizo za kigeni

/ Published posts: 1905

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram