

Mawasiliano ya Barabara Somanga – Mtama yameanza kurejea kwa hatua katika barabara iendayo mikoa ya Kusini tangu leo alfajiri baada ya wataalamu wa Wakala wa Barabara (TANROADS) kufanya kazi usiku na mchana kurekebisha eneo la Somanga na Matandu lililoharibiwa na mvua na kufanya njia isipitike.
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ambaye ameweka kambi katika eneo hilo tangu jana, amewaambia waandishi wa habari kwamba magari madogo 230, mabasi 10 na baadhi ya malori 30 yaliyobeba bidhaa mbalimbali ikiwemo mawe makubwa yamefanikiwa kuruhusiwa kupita katika eneo la Somanga Mtama na Matandu kuanzia leo kati ya saa 11:30 alfajiri hadi saa 12:00 asubuhi.

Ulega ameyasema hayo leo wakati akitoa taarifa ya awali akiwa mkoani Lindi wakati akiendelea kusimamia zoezi la urejeshaji wa maeneo yaliyokatika katika barabara kuu ya Dar es Salaam – Lindi linaofanywa na Timu ya Wizara ya Ujenzi na Wakala wa Barabara (TANROADS) kwa kushirikiana na Mkandarasi.
Baadhi ya abiria waliolazimika kusubiri usafiri usiku kucha wamezungumza na waandishi wa habari na kutoa shukrani kwa wataalamu waliofanikisha kazi hiyo kwa kufanya kazi usiku kucha.

“Tunaishukuru sana serikali hasa wataalamu wake na mheshimiwa Waziri wa Ujenzi ambaye tumeshinda naye hapa kutwa nzima mpaka jioni na akatuahidi leo tutaondoka na neno lake limetimia,” alisema Shaaban Matwanga mkazi wa Lindi ambaye ameondoka kwenda Dar es Salaam leo.
Katika maelezo yake, Ulega alisema matengenezo zaidi katika maeneo ya Somanga Mtama na Matandu yanaendelea kuimarishwa kwa kuendelea kuwekwa mawe makubwa ili kuruhusu na magari mengine yaliyobakia kupita.

Ulega amewahakikishia Watanzania kuwa serikali ipo kazini usiku na mchana katika kuhakikisha miundombinu ya barabara hiyo inaimarishwa ili isiwe kikwazo kwa wasafiri.